Dec 01, 2025 02:44 UTC
  • Jumatatu, Mosi Disemba, 2025

Leo ni Jumatatu tarehe 10 Mfunguo Tisa Jamaduthani 1447 Hijria mwafaka na Mosi Disemba 2025.

Miaka 820 iliyopita katika siku kama hii ya leo aliaga dunia arifu na malenga mashuhuri wa Kiislamu na Kiirani Fariduddin Attar Naishaburi.

Attar Naishaburi alizaliwa karibu mwaka 513 Hijria Qamaria katika eneo la Naishabur na baada ya kufariki dunia baba yake ambaye alikuwa muuza madawa, aliendeleza kazi hiyo ya baba na kupata maarifa mengi kuhusu elimu ya tiba. Katika kipindi hicho alipatwa na mabadiliko makubwa na kuanza safari ya ndani ya nafsi na kutakasa roho. Alifanya safari katika maeneo mengi ya Ulimwengu wa Kiislamu na kupata elimu ya irfani kwa wanazuoni wakubwa wa zama hizo.

Attar Naishaburi ameandika tajiriba na uzoefu wake wa kiirfani katika kalibu ya mashairi na nathari. Miongoni mwa vitabu vya arifu huyo mkubwa Muirani ni "Tadhkiratul Auliyaa" na "Mantiqut Twair."

Mahali lilipo kaburi la Attar Naishaburi

Katika siku kama ya leo miaka 200 iliyopita, muungano wa kihistoria wa nchi za Ulaya uliojulikana kama Muungano Mtakatifu ulisambaratika baada ya kujiengua utawala wa Kikaitsar (Tsarist) wa Russia katika muungano huo.

Baada ya kuanguka kwa utawala wa Napoleon, muungano huo ukaunda Congress ya Vienna, kati ya tawala za Russia, Austria na ufalme wa Pros na serikali hizo zikaafikiana kwamba nchi zilizo chini ya utawala wa muungano huo na katika uhusiano wa kimataifa zifuate misingi ya dini ya Kikristo. 

Siku kama hii ya leo miaka 87 iliyopita Ayatullah Sayyid Hassan Mudarres, mwanazuoni mwanamapambano na mpigania ukombozi wa Kiirani aliuawa shahidi na vibaraka wa Reza Khan, mtawala dhalimu wa Iran wa wakati huo katika mji wa Kashmar kaskazini mashariki mwa Iran.

Ayatullah Sayyid Hassan Mudarres aliamua kuanzisha mapambano dhidi ya utawala huo baada ya kujionea dhulma na ukandamizaji wa mtawala Reza Khan nchini Iran. Alifanya jitihada kubwa za kutekelezwa sheria za Kiislamu hapa nchini na kuiokoa Iran kutoka kwenye makucha na udhibiti wa wakoloni.

Kwa msingi huo mtawala kibaraka wa wakati huo wa Iran, Reza Khan Pahlavi alimuona kuwa adui mkubwa na kuchukua uamuzi wa kumuua.   

Sayyid Hassan Mudarres

Siku kama ya leo miaka 52  iliyopita David Ben-Gurion mmoja wa waasisi wa utawala wa Kizayuni wa Israel na Waziri Mkuu wa kwanza wa utawala huo ghasibu aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 87.

Ben-Gurion alizaliwa tarehe 16 Oktoba 1886 katika mji wa Plonsk huko Poland ambayo katika zama hizo ilikuwa sehemu ya ardhi ya ufalme wa Russia. Alielekea katika ardhi za Palestina mwaka 1906 akiwa na umri wa miaka 20 na kuasisisi harakati ya Kiyahudi.

Katika Vita vya Kwanza vya Dunia David Ben-Gurion alikuwa na nafasi kubwa katika kuwahamisha taratibu Mayahudi kwenda ardhi za Palestina. Katika kipindi cha Vita vya Pili vya Dunia harakati hiyo ilishika kasi chini ya uungaji mkono wa madola makubwa hususan Uingereza, kiasi kwamba mwaka 1948 sawa na tarehe 5 Mei na baada ya kupitishwa azimio na Umoja wa Mataifa la kuigawa Palestina katika pande mbili za Kiyahudi na Palestina, kulitangazwa rasmi kuanzishwa utawala haramu wa Kizayuni na wa kibaguzi wa Israel.

Masaa machache baadaye, Marekani na Urusi ya zamani zikatangaza kuutambua utawala huo khabithi.

David Ben-Gurion

Na tarehe Mosi Disemba kila mwaka, nchi mbalimbali duniani huadhimisha Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Ukimwi.

Ukimwi ni ugonjwa wa kuambukiza ambao unatokana na kurundikana kwa virusi vya HIV mwilini ambavyo huharibu mfumo wa ulinzi wa mwili na kutayarisha mazingira ya kushambuliwa na maradhi nyemelezi. Ugonjwa huu ulibainika kwa mara ya kwanza kabisa nchini Marekani mwazoni mwa miaka ya 1980. Wakati huo baadhi ya wanaume wanaofanya ngono kinyume na maumbile huko New York na California waligundulika kuwa na kansa ambazo hazikukubali tiba ya aina yoyote.

Japokuwa wakati huo, haikujulikana sababu ya maambukizi ya ghafla ya magonjwa hayo lakini tukio hilo limetambuliwa kuwa ndiyo mwanzo wa kujitokeza maradhi ya Ukimwi. Ugonjwa huo ambao haukuwa na jina ulienea kwa kasi kubwa katika kipindi cha mwaka mmoja na hatimaye mwaka 1982 ulipewa jina la Ukimwi.