Jumatano, Novemba 27, 2024
Leo ni Jumatano tarehe 25 Mfunguo Nane Jamadil Awwal 1446 Hijria inayosadifiana na tarehe 27 Novemba 2024 Milaadia.
Tarehe 27 Novemba miaka 105 iliyopita iliainishwa mipaka mipya ya nchi za Ulaya na Mashariki ya Kati baada ya kumalizika Vita vya Kwanza vya Dunia.
Baada ya kumalizika vita hivyo na kutiwa saini mkataba wa amani wa Versailles kulisainiwa mikataba mingine kadhaa ya kuainisha mustakabali wa tawala za Austria na Hungary na utawala wa Othmania na nchi ya Bulgaria ambayo kila mmoja ulikuwa na masharti mazito na kutoa fidia nchi hizo kwa zile zilizopata ushindi.
Kuainishwa kwa mipaka mipya ya nchi za Ulaya na Mashariki ya Kati katika mkutano wa Paris kulibadili kikamilifu ramani ya dunia.
Katika siku kama ya leo miaka 81 iliyopita, mkutano wa siku 3 wa viongozi wa Marekani, Uingereza na Umoja wa Sovieti ulifanyika mjini Tehran katika hali ambayo, Iran wakati huo ilikuwa chini ya uvamizi wa majeshi ya nchi hizo.
Mkutano wa Tehran ulifanyika baada ya Marekani kuingia katika Vita vya Pili vya Dunia na kuzuka kambi mpya dhidi ya jeshi la Ujerumani.
Walioshiriki katika mkutano huo walikuwa Rais Franklin Delano Roosevelt wa Marekani, Waziri Mkuu wa Uingereza, Winston Churchill na Joseph Stalin kiongozi wa wakati huo wa Umoja wa Kisovieti. ***
Miaka 71 iliyopita katika siku kama ya leo aliaga dunia Eugene O’Neill mwandishi Kimarekani. Eugene O’Neill ambaye alikuwa mashuhuri pia katika uandishi wa tamthilia aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 65. Alizaliwa mwaka 1888 na maisha yake yalitawaliwa na matukio mengi. Eugene O’Neill alikuwa na mapenzi makubwa na tamthilia na ndio maana akapewa jina la mtoto wa tamthilia. Mwaka 1936 Eugene O'Neill alitunukiwa tuzo ya Nobel. Baadhi ya vitabu vya mwandishi huyu ni Mfalme Jones, The First Man na Days Without Ends.
Katika siku kama ya leo 44 iliyopita, vikosi vya majini vya Iran vilifanya operesheni katika maji ya Ghuba ya Uajemi na kufanikiwa kuvisambaratisha vikosi vya majini vya Iraq.
Tukio hilo lilitokea takribani miezi miwili tu baada ya kuanza vita vya kichokozi vya Iraq dhidi ya Iran. Operesheni hiyo ilipelekea kutokea mapigano makali kati ya meli za kivita za pande mbili na meli nyingi za kivita za Iraq ziliteketezwa. Kutokana na ushujaa wa wapiganaji wa vikosi vya majini katika operesheni hiyo, siku hii inajulikana hapa nchini kwa jina la “Siku ya Jeshi la Majini”.
Na siku kama ya leo miaka 4 iliopita Mohsen Fakhrizadeh Mahabadi aliyekuwa Naibu Waziri wa Ulinzi wa Iran aliuawa shahidi katika hujuma ya kigaidi.
Mohsen Fakhrizadeh alizaliwa mwaka 1336 Hijria Shamsia huko Qum na alikuwa mwanachama wa Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sepah) tangu lilipoundwa. Alitambulia kuwa msomi wa ngazi za juu wa Wizara ya Ulinzi na Kituo cha Utafiti wa Fizikia hapa nchini (PHRC).
Shahidi Fakhrizadeh alikuwa na mchango mkubwa sana katika juhudi za pamoja za Wizara ya Afya na Wizara ya Ulinzi ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran za kuzalisha vifaa vya kupambana na maambukizi ya corona ikiwa ni pamoja na kuzalisha chanjo ya virusi hivyo.
Hatimaye Ijumaa ya tarehe 7 Azar 1399 (27 Novemba 2020) aliuawa shahidi katika hujuma iliyotekelezwa eneo la Absard na kupata daraja ya juu ya kuuliwa shahidi. Waziri wa Mambo ya Nje wa wakati huo wa Iran alisema kuna ushahidi madhubuti unaothibitisha kuwa Israel ilihusika na mauaji hayo ya kigaidi.