Aug 05, 2016 06:10 UTC
  • Ijumaa tarehe 05 Agosti 2016

Leo ni Ijumaa tarehe Pili Dhulqaada 1437 Hijria sawa 5 Agosti 2016.

Miaka 1126 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Ibn Khuzaima, mpokeaji wa hadithi na faqih mashuhuri wa karne ya nne Hijria. Ibn Khuzaima alizaliwa mwaka 223 Hijria na alifanya safari katika pembe mbalimbali duniani wakati wa ujana wake kwa lengo la kujipatia elimu mbalimbali za kidini. Faqihi huyo wa Kiislamu ameandika vitabu vingi vya thamani kikiwemo kile alichokiita Attauhid fii It'abati Sifati Rabb «التوحید و اثبات صفات الرب».

Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 5 Agosti 1960, nchi ya Burkina Faso iliyoko magharibi mwa Afrika ilipatia uhuru. Burkina Faso ilikuwa chini ya mkoloni Mfaransa tokea katikati mwa karne ya 19. Nchi hiyo ambayo zamani ilikuwa ikijulikana kwa jina la Upper Volta, ilianza kujipatia mamlaka ya ndani mwaka 1958, lakini miaka miwili baadaye ilipatia uhuru kamili na kuwa mwanachama wa Umoja wa Mataifa. Hata hivyo, ilipofika mwaka 1984, nchi hiyo iliamua kubadilisha jina kutoka Upper Volta na kuitwa Burkina Faso. Nchi hiyo ya Kiafrika inapakana na nchi za Mali, Ivory Coast, Ghana, Togo, Benin na Niger.

Tarehe 5 Agosti mwaka 121 iliyopita, alifariki dunia Friedrich Engels mwanafalsafa mashuhuri wa Ujerumani. Alikuwa rafiki na mshirika wa karibu wa mwanafalsafa mwingine wa Ujerumani yaani Karl Marx. Engels alifuatiliwa na kusakwa na vyombo vya dola kutokana na harakati zake za kisiasa na mwaka 1850 alikimbilia nchini Uingereza. Engels na Karl Marx walitayarisha Manifesto ya Ukomonisti iliyotangazwa na vyama vya kikomonisti katika mkutano wao wa kwanza mnamo mwaka 1848. Baada ya Karl Marx, Friedrich Engels alikuwa na nafasi muhimu katika kujitokeza nadharia ya ukomonisti.

Na tarehe 15 Mordad miaka 28 iliyopita dikteta wa zamani wa Iraq, Saddam Hussein alilazimika kukubali usitishaji vita baina ya Iraq na Iran. Baada ya Iran kukubali azimio nambari 598 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ambalo lilisisitiza udharura wa kusimamishwa vita baina ya pande hizo mbili, ilitazamiwa kuwa mapigano yangesitishwa baina ya pande hizo mbili. Hata hivyo siku kadhaa baadaye Saddam alianzisha mashambulizi makubwa dhidi ya Iran ambayo yalifeli kutokana na ushujaa mkubwa wa wapiganaji wa Kiislamu wa Iran. Hatimaye na baada ya vita vya miaka 8 Saddam alilazimika kusitisha vita vilivyosababisha hasara kubwa ya mali na nafsi kwa mataifa mawili jirani ya Iran na Iraq.

Miaka 26 iliyopita katika siku kama hii ya leo kikao cha 19 cha Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) ambayo ilikuwa ikiitwa Jumuiya ya Nchi za Kiislamu kilichofanyika mjini Cairo Misri, kulipasisha hati ya "Haki za Binadamu za Kiislamu" na siku hiyo ikatambuliwa kwa jina la siku ya "Haki za Binadaamu za Kiislamu na Utukufu wa Mwanadamu." Hati hiyo ina utangulizi na vipengee 25. Baada ya Umoja wa Mataifa kuutangazia ulimwengu haki za binadaamu mwaka 1948, nchi nyingi za dunia zilitangaza kuwa, haki hizo zilikuwa zimeandikwa kwa mujibu wa misingi ya kiliberali na kisekula ya Magharibi na kwamba sheria hizo haziendani na utamaduni wa nchi hizo hususan zile za Kiislamu.

Na siku kama ya leo miaka 53 iliyopita mkataba wa kuzuia majaribio ya silaha za nyuklia kati ya Marekani, Urusi ya zamani na Uingereza ulitiwa saini. Baada ya kuanza kipindi cha Vita Baridi, ulimwengu ulikaribia kutumbukia katika vita vikubwa vya maangamizi kutokana na kuanza majaribio ya nyuklia na utengenezaji wa makombora yanayovuka mabara na yenye vichwa vya silaha za nyuklia. Suala la Cuba na kupelekwa huko makombora ya Urusi lilifikisha mgogoro huo kileleni. Baada ya kusainiwa mkataba huo anga ya kimataifa ilitulia kidogo na kukaanza mazungumzo ya jadi kwa ajili ya kusimamisha majaribio ya silaha za nyuklia. Kuanzia Oktoba mwaka 1958 Marekani, Urusi na Uingereza zilitilia maanani suala la kusitisha majaribio ya silaha hizo japokuwa ziliendelea kufanya majaribio hayo. Hatimaye na baada ya mazungumzo mapana, nchi hizo tatu zilifikia makubaliano ya kuzuia majaribio ya silaha za nyuklia ambayo yalitiwa saini tarehe 5 Oktoba mwaka 1963.