Aug 16, 2016 04:28 UTC
  • Jumanne, Agosti 16, 2016

Leo ni Jumanne tarehe 13 Dhilqaada 1437 Hijria sawa na 16 Agosti 2016.

Siku kama leo miaka 128 iliyopita, alizaliwa Thomas Edward Lawrence, jasusi mkubwa wa Uingereza aliyekuwa na mchango mkubwa katika kuzidhoofisha nchi za Kiarabu. Kabla ya Vita vya Kwanza vya Dunia Lawrence, alikuwa amefanya safari katika nchi kadhaa za Kiarabu, ambapo sanjari na kujifunza lugha ya Kiarabu, alifahamu pia tamaduni na maisha ya Waarabu. Katika vita hivyo vya Kwanza vya Dunia vilivyojiri kati ya mwaka 1914 hadi 1918, na kwa msingi wa siasa za kikoloni za Uingereza, Lawrence alifanya njama kubwa kuyachochea makabila ya Kiarabu kwa kisingizio cha kutaka kujitawala, ili yaweze kujitenga na utawala wa Othmania ambao katika vita hivyo ulikuwa ukikabiliana na Uingereza. Thomas Edward Lawrence pia alikuwa na nafasi muhimu katika kuuingiza madarakani ukoo wa Aal-Saud nchini Saudia, suala ambalo lilipelekea kupata umashuhuri mkubwa nchini Saudia.

Siku kama ya leo miaka 56 iliyopita, kisiwa cha Cyprus kilipata uhuru baada ya machafuko ya miaka kadhaa. Kisiwa hicho ambacho hii leo kinaendeshwa chini ya mfumo wa jamhuri, kiko katika bahari ya Mediterraneanna kusini mwa Uturuki kikiwa na ukubwa wa zaidi ya kilomita mraba 9000. Kwa miaka kadhaa kisiwa cha Cyprus chenye historia kongwe na muhimu katika eneo kilikuwa chini ya falme za Iran, Ugiriki, Misri na utawala wa Othmania. Lakini mwaka 1878, utawala wa  Othmania ulikabidhi usimamizi wa kisiwa hicho kwa Uingereza katika mkutano uliofanyika mjini Berlin Ujerumani na mwaka 1925 kisiwa cha Cyprus kikawa rasmi koloni la Uingereza.

Tarehe 26 Mordad miaka 35 iliyopita aliuawa Mulla Salih Khosravi, mwanazuoni wa Kisuni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Msomi hiyo aliuawa na vibaraka wanaopinga Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini. Mulla Khosravi alikuwa miongoni mwa wanazuoni wa madhehebu ya Suni waliosimama kupambana na utawala wa Shah, kutetea Uislamu na kuhubiri umoja baina ya Waislamu nchini Iran kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na alipata mateso mengi na kufungwa jela mara ngingi.

Na siku kama ya leo miaka 13 iliyopita, Idi Amin Rais wa zamani wa Uganda alifariki dunia. Idi Amin aliyekuwa Rais wa tatu wa Uganda aliaga dunia katika hospitali moja nchini Saudi Arabia alikokuwa uhamishoni. Alizaliwa mwaka 1925 Kaboko jirani na Arua kaskazini magharibi mwa Uganda. Idi Amin aliiongoza Uganda kuanzia mwaka 1971 hadi 1979. Inasemekana kipindi cha utawala wake nchini Uganda kiliambatana na mauaji na ukiukaji wa haki za binadamu. Idi Amin Dada aliondolewa madarakani nchini Uganda na vikosi vya jeshi vya Tanzania mwaka 1979 pamoja na Waganda waliokuwa uhamishoni.