Jan 30, 2026 02:46 UTC
  • Ijumaa, tarehe 30 Januari, 2026

Lo ni Ijumaa tarehe 10 Sha'ban 1447 Hijria inayosadifiana na tarehe 30 Januari 2026.

Siku kama ya leo miaka 1025 iliyopita, yaani tarehe 10 Shaaban mwaka 422 Hijria, aliaga dunia Abu Abdullah Abdulbaqi, mmoja wa malenga mashuhuri wa karne ya tano Hijria.

Alikuwa akiishi katika mji wa Baghdad, ilipo Iraq ya sasa. Mbali na kupata elimu kwa malenga na wanafasihi wakubwa, Abdulbaqi alikuwa akihudhuria pia darsa za maulamaa watajika wa mji huo katika zama hizo na kufaidika kwa elimu mbalimbali hasa elimu ya Hadithi.

Abu Abdullah Abdulbaqi alikuwa na kipaji cha maumbile cha kusanifu mashairi na ameacha athari nyingi katika uga huo. ***

Miaka 693 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 10 Shaaban mwaka 754 Hijria aliaga dunia Majdu-ddin Abul Fawaaris, mmoja wa maulamaa wakubwa wa Kiislamu.

Alizaliwa nchini Iraq; na baada ya kuhitimu masomo yake ya msingi alikamilisha masomo yake ya dini kwa maulamaa wakubwa, mpaka yeye mwenyewe akafikia daraja ya kuwa alimu mwenye wanafunzi walio chini yake. Alichota elimu nyingi katika fani za Fiqhi, Usul-Fiqhi, Hadithi, Ilmul-Kalam, Tafsiri ya Qur'ani na Fasihi ya Kiarabu.

Mwanazuoni huyo mkubwa wa Kiislamu ameacha athari nyingi, miongoni mwazo ni kitabu kiitwacho Kanzul-Fawaaid. ***

Siku kama ya leo miaka 92 iliyopita, kilianza kipindi cha uongozi wa Adolph Hitler, dikteta mbaguzi wa Kinazi wa Ujerumani.

Chama cha Taifa cha Kisoshalisti cha Wafanyakazi wa Ujerumani ambacho kiliasisiwa na Hitler kilishinda viti 107 vya bunge katika uchaguzi wa mwaka 1930. Adolph Hitler alijitangaza kuwa kiongozi wa Ujerumani mwaka 1934 baada ya kuwa Kansela na Rais wa nchi hiyo.

Hitler aliwafanya mamilioni ya wanadamu kuwa wahanga wa malengo yake ya kibaguzi. Hatua ya Adolph Hitler ya kuivamia Poland mwezi Septemba mwaka 1939 ilichochea Vita vya Pili vya Dunia na hatimaye Ujerumani na waitifaki wake walishindwa katika vita hivyo.

Hitler alijiua mwaka 1945 baada ya Ujerumani kushindwa katika vita hivyo. ***

Katika siku kama ya leo miaka 78 iliyopita kiongozi wa taifa la India na mpigania uhuru wa nchi hiyo, Mohandas Karamchand Gandhi aliuawa na kijana mmoja wa Kihindu aliyekuwa na misimamo mikali.

Gandhi alizaliwa mwaka 1869 na baada ya kukamilisha masomo alitunukiwa shahada ya digrii katika taaluma ya sheria nchini Uingereza. Mohandas Gandhi kwa muda fulani pia alikuwa kiongozi wa wanamapambano wa Kihindi huko Afrika Kusini.

Gandhi pia aliwaongoza wananchi wa India dhidi ya serikali ya kikoloni ya Uingereza katika kupigania ukombozi wa nchi hiyo. India ilipata uhuru mwaka 1947 chini ya uongozi wa Gandhi. ****

Katika siku kama ya leo miaka 77 iliyopita Orville Wright, mmoja wa waundaji wa ndege ya kwanza inayotumia injini duniani, alifariki dunia. 

Orville alizaliwa mnamo Agosti 19, 1871 katika jimbo la Ohio huko Marekani na alikuwa mdogo kwa miaka minne kuliko kaka yake, Wilbur. Orville na Wilbur walikuwa watoto wa padri ambaye hakuweza kumudu gharama za masomo yao kutokana na umaskini. Kwa hivyo, ndugu hawa wawili, ambao walivutiwa na kazi za ufundi na utengenezaji wa injini na mashine, walianzisha warsha ya kutengeneza baiskeli. 

Ndugu hawa wawili, ambao walikuwa na hamu kubwa ya kuruka angani, hatimaye walitimiza ndoto yao ya muda mrefu mnamo Desemba 17, 1903, na wakavumbua ndege ya kwanza yenye injini ulimwenguni ambayo iliruka angani kwa sekunde 59.  ***