Oct 22, 2026 06:05 UTC
  • Alkhamisi, Oktoba 22, 2026

Leo ni Alkhamisi mwezi 11 Mfunguo Nane, Jumada al-Ula 1448 Hijria, sawa na tarehe 22 Oktoba, 2026 Miladia

Miaka 851 iliyopita, yaani mwezi 11 Jumada al-Ula, mwaka 597 Hijria alizaliwa katika mji wa Tus ulioko kaskazini mashariki mwa Iran Khwaja Nasiir al-Din Tusi, mwanafalsafa, mwanahisabati, astronomia, mwanafizikia, msanifu majengo na mwanasayansi mkubwa wa Kiirani. Khwaja Nasiir alikuwa mmoja wa shakhsia mashuhuri na mwenye taathira kubwa katika historia ya Iran. Alisomeshwa fiqhi na Hadithi na baba yake na mantiki na hikma na mjomba wake. Baada ya hapo Khwaja Nasiir akaelekea Nishapur kaskazini mashariki mwa Iran ambako alijifunza elimu mbalimbali za zama zake, ikiwemo hisabati na unajimu kwa kiwango cha kutabahari kwa maulamaa wakubwa wa mji huo. Katika zama za utawala wa Mongol Hulagu Khan na mwanawe, Khwaja Nasiir alianzisha kituo kikubwa cha kisayansi na akademia ya kwanza ya sayansi, iitwayo Kituo cha Kuangalilia jua, nyota na mwezi cha Maragheh, kwa kimombo Observatory. Khwaja Nasir al-Din aligundua mbinu mpya za kutumia saa ya jua kwa ajili ya uangaliliaji wake. Kwa juhudi zake, Kituo hicho cha uchunguzi cha Maragheh kilijaa vifaa bora kabisa vya uchunguzi, ambavyo havikupatikana mfano huko Magharibi hata baada ya miaka 300 baadaye. Kando yake kituo hicho, Khwaja Nasir al-Din Tusi alijenga maktaba yenye vitabu zaidi ya 4,000. Kwa muda wa miaka 16, alitalii na kufanya utafiti wa nyota katika kituo hicho cha uchunguzi cha Maraghe. Mwanasayansi huyo mtajika, mbobezi na mchapakazi wa Kiirani ameacha vitabu na makala zaidi ya 80 vya lugha ya Kiarabu na Kiajemi vikiwemo "Asasul-Iqtibaas", "Akhlaqu Naasiri", "Awsaful-Ashraf" na "Sharhe Ishaarate Ibn Sina". Khwaja Nasir al-Din Tusi aliaga dunia mwaka 672 hijria na akazikwa katika mji wa Kadhimiyyah nchini Iraq.

&&&

Miaka 120 iliyopita katika siku kama ya leo, Paul Cezanne mchoraji maarufu wa Kifaransa aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 67.

Tangu utotoni mwake, Cezanne alikuwa na shauku kubwa ya fani ya uchoraji, lakini kutokana na msisitizo wa baba yake aliingia Chuo Kikuu na kusomea taaluma ya sharia.

Hatimaye akiwa na umri wa miaka 24, baba yake alimruhusu aende Paris akaendelee na masomo katika fani ya uchoraji. Mwanzoni mabango ya michoro ya Paul Cezanne hayakutoa mvuto kwa watu na athari zake za uchoraji zilikosolewa sana. Hali hiyo iliendelea hadi alipotimia umri wa miaka 50 ambapo alianza kidogokidogo kupata umashuhuri kwa kuuza mabango ya michoro yake.   

&&&

Miaka 74 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 30 Mehr 1331 kwa kalenda ya Hijria Shamsia, Dakta Hussein Fatemi, Waziri wa Mambo ya Nje wa serikali ya Dakta Mohammad Musaddegh, aliyekuwa Waziri Mkuu wa Iran wakati huo alitangaza habari ya kuvunjwa uhusiano wa kisiasa kati ya Iran na Uingereza.

Uamuzi huo ulikabidhiwa kwa balozi mdogo wa Uingereza mjini Tehran, baada ya kuidhinishwa na baraza la mawaziri.

Dakta Fatemi alisema Tehran imeamua kuvunja uhusiano na Uingereza kutokana na serikali ya London kutojali matakwa ya wananchi wa Iran ya kupata haki zao, hususan katika suala la kutaifisha sekta ya mafuta. Dakta Fatemi aliwataka viongozi wa London wabadilishe sera zao kuhusiana na Iran.   

&&&

Siku kama ya leo miaka 51 iliyopita, aliaga dunia Arnold Joseph Toynbee mwanahistoria mtajika wa Uingereza.

Alizaliwa mwaka 1889. Toynbee alikuwa akifundisha taaluma ya Historia ya Kimataifa katika Chuo Kikuu cha London.

Msomi huyo ameandika vitabu vingi katika uga wa historia na baadhi ya vitabu vyake ni A Study of History, Change and Habit, Choose Life na Civilization on Trial.     

&&&

Na miaka 15 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Sultan bin Abdul-Aziz Aal Saud aliyekuwa mrithi wa kiti cha Ufalme wa Saudia.

Sultan alikuwa mtoto wa 15 wa kiume wa Mfalme Abdul-Aziz, na mama yake ni Hussa Bint Ahmed Al-Sudairi. Vyombo vya Saudi vilitangaza kuwa, mwanamfalme Sultan bin Abdul-Aziz Aal Saud aliaga dunia katika hospitali moja mjini New York, Marekani. Sultan bin Abdul-Aziz alifariki akiwa na umri wa miaka 85 baada ya maradhi ya saratani kuenea mwilini mwake. 

&&&