Jumatano, Oktoba 21, 2026
-
Leo Katika Historia
Leo ni Jumatano mwezi 10 Mfunguo Nane, Jumada al-Ula 1448 Hijria, sawa na tarehe 21 Oktoba, 2026 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 236 iliyopita, alizaliwa malenga wa Kifaransa, Alphonse de Lamartine.
De Lamartine alitambulika kama msanii na mwanafikra mkubwa nchini Ufaransa. Aliwahi pia kusafiri kuelekea ulimwengu wa Mashariki na kuishi katika mji mkuu wa Lebanon, Beirut. Miongoni mwa athari za malenga huyu, ni pamoja na "Safari ya Mashariki" na "Kimya cha Malaika".
Alphonse de Lamartine alifariki dunia mwaka 1869.
&&&
Siku kama ya leo miaka 123 iliyopita alifariki dunia Ayatullah Sayyid Ismail Nuri Tabarsi, faqihi, mtaalamu mkubwa wa elimu ya teolojia na Hadithi. Ayatullah Sayyid Ismail Nuri Tabarsi alizaliwa katika mji wa Mazandaran, nchini Iran mwanzoni mwa karne ya 13 Hijiria Shamsia katika moja ya vijiji vya kaunti ya Nur. Baada ya kuhitimu masomo ya msingi alijiunga na chuo cha kidini na baadaye akaelekea Najaf, Iraq kwa ajili ya kuendelea na masomo ya juu. Akiwa Najaf alisoma masomo ya ngazi ya juu ya fiqhi, usulul- fiqhi, teolojia na Hadithi kwa maulama wakubwa kama Sheikh Morteza Answari, Mirza Habibullah Rashti na Mirza Mohammad Hassan Shirazi maarufu kwa jina la Mirza Mkubwa. Mbali na kujishughulisha na kazi ya ufundishaji, aliandika pia vitabu vya thamani kama vile 'Kifaayatul-Muwahhidin' chenye juzuu tatu. Msomi huyo alifariki dunia mjini Kadhimiya, Iraq na kuzikwa huko.
&&&
Miaka 193 iliyopita katika siku kama ya leo, alizaliwa Alfred Nobel mkemia wa Sweden na mvumbuzi wa dynamite.
Nobel alikuwa na shauku kubwa ya kujifunza sayansi ya kemia na baadaye akafanya utafiti mkubwa katika uwanja huo na kufanikiwa kuvumbua mada hizo za mripuko yaani (dynamite). Kinyume na alivyotarajia, majeshi ya nchi mbalimbali yalianza kutumia dynamite vitani na hivyo kusababisha mauaji ya raia wengi.
Mkemia Nobel ambaye alikuwa na utajiri mkubwa na hakufikiri kuwa dynamite ingeweza kutumiwa vibaya, aliamua kutoa utajiri wake kama tuzo na zawadi. Alfred Nobel alifanya hivyo kwa lengo kwamba, tuzo hiyo itolewe kila mwaka kwa shakhsiya aliyefanya kazi kubwa ya thamani duniani katika masuala ya sayansi, fasihi na amani.
Hata hivyo kinyume na matakwa yake, leo hii Tuzo ya Amani ya Nobel imechukua sura ya kisiasa na inatumiwa kama wenzo wa kutangaza na kueneza siasa za nchi za Magharibi duniani.
&&&
Katika siku kama ya leo miaka 66 iliyopita, nchi ya Kiafrika ya Somalia ilipata uhuru na siku hii inajulikana nchini humo kama Siku ya Taifa.
Kijiografia Somalia ipo kaskazini mashariki mwa bara la Afrika katika eneo linalojulikana kama Pembe ya Afrika. Mji mkuu wa Somalia ni Mogadishu na lugha rasmi ya nchi hiyo ni Kisomali na Kiarabu. Asilimia 99 ya wananchi wa Somalia ni Waislamu.
Nchi hiyo kwa miaka kadhaa ilikuwa chini ya ukoloni wa Italia na Uingereza mpaka ilipojipatia uhuru mwaka 1960 katika siku kama ya leo.
&&&