Jumamosi, Aprili 29, 2017
Leo ni Jumamosi tarehe Pili Shaaban 1438 Hijria sawa na tarehe 29 Aprili 2017 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1042 iliyopita sawa na tarehe Pili Shaaban 396 Hijria, alizaliwa Khwaja Abdullah Ansari, faqihi, malenga na 'arif mtajika katika mji wa Herat magharibi mwa Afghanistan. Khwaja Abdullah Ansari ameacha vitabu vingi mashuhuri vya kiirfani ambavyo vimeandikwa kwa lugha za Kiarabu na Kifarsi, ikiwa ni pamoja na 'Munajaat Naame', 'Mahabbat Naame' na 'Zaadul 'Arifiin'. Msomi na malenga huyo mashuhuri katika karne ya tano Hijria alifariki dunia mwaka 481 Hijjria. ***
Miaka 163 iliyopita katika siku kama ya leo, Henri Poincare mtaalamu wa sayansi na hisabati wa Ufaransa alizaliwa katika mji wa Nancy nchini humo. Poincare alikuwa mahiri katika somo la hisabati na alijihusisha na kufanya utafiti katika uwanja huo. Tafiti mbalimbali zilizofanywa na mwanahisabati huyo wa Kifaransa kuhusiana na masuala ya uchanganuzi wa kimahesabu, mwangaza, umeme n.k zimetajwa kuwa muhimu na sahihi. Msomi huyo alianda vitabu kadhaa katika nyanja mbalimbali za elimu. ***
Katika siku kama ya leo miaka 89 iliyopita, sawa na tarehe 29 mwezi Aprili mwaka 1928, nchini Uturuki herufi za Kilatini zilitambuliwa rasmi na kuchukua nafasi ya zile za Kiarabu. Hatua hiyo ilichukuliwa katika njama za kuipiga vita dini ya Uislamu na badala yake kuingizwa tamaduni za Kimagharibi katika jamii ya wananchi wa Uturuki. Mchakato huo ulianzishwa na Mustafa Kamal maarufu kwa jina la Ataturk kuanzia mwaka 1923. Mfumo wa Jamhuri ulishika hatamu za uongozi huko Uturuki chini ya Ataturk kuanzia mwezi Oktoba mwaka 1923 baada ya kuanguka kwa utawala wa Othmania uliodumu kwa miaka 623 nchini humo. ***
Siku kama ya leo miaka 72 iliyopita, majeshi ya waitifaki yalipata pigo kubwa mwishoni mwa Vita vya Pili vya Dunia. Vikosi vya nchi Waitifaki wa Ulaya vilifanya mashambulizi ya pande zote dhidi ya Italia baada ya kusambaratishwa safu ya ulinzi ya Ujerumani. Italia ilikuwa muitifaki wa Ujerumani chini ya uongozi wa Benito Mussolini. Baada ya ushindi huo askari karibu milioni moja wa Ujerumani waliokuwa nchini Italia walijisalimisha kwa majeshi ya Waitifaki. ***
Katika siku kama ya leo miaka 26 iliyopita, mwafaka na siku kama hii ya leo alifariki dunia Dakta Ghulam Hussein Sidiqi akiwa na umri wa miaka 78. Alikuwa mwalimu, mhakiki na mtaalamu wa elimu jamii wa Kiirani. Dakta Hussein Sadiqi alihitimu masomo yake katika vyuo mbalimbali vya elimu na katika shule ya Dar ul- Funun ya mjini Tehran. Dakta Sidiqi alienda Ufaransa kwa ajili ya kuendelea na masomo ya elimu ya juu na baada ya kufikia daraja ya udaktari katika taaluma za historia, falsafa na elimu ya jamii, alirejea Iran na kujishughulisha na kazi ya kufundisha katika Chuo Kikuu cha Tehran. Dakta Ghulam Hussein Sidiqi hakuwa nyuma pia katika uwanja wa uandishi vitabu. Miongoni mwa vitabu vyake ni kile cha "Ripoti ya Safari ya India" "Sherehe za Kidini za Kiirani Katika Karne ya Pili na Tatu Hijria" na "Tas'hih Risalati Ibn Sina."
Na miaka 18 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 9 Ordibehesht mwaka 1378 Hijria Shamsia, wawakilishi wa duru ya kwanza ya "Mabaraza ya Kiislamu ya Miji na Vijiji" nchini Iran walianza kazi zao na siku hii inajulikana hapa nchini kwa jina la "Siku ya Mabaraza".