UN yaongeza muda wa kuhudumu askari AUSSOM nchini Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i134692-un_yaongeza_muda_wa_kuhudumu_askari_aussom_nchini_somalia
Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha kwa kauli moja azimio la kuongeza muda wa Ujumbe wa Umoja wa Afrika wa Msaada na Kurejesha utulivu nchini Somalia (AUSSOM) kwa mwaka mmoja zaidi, hadi tarehe 31 Desemba 2026.
(last modified 2026-02-21T22:51:18+00:00 )
Dec 24, 2025 23:08 UTC
  • Askari wa AUSSOM, Somalia
    Askari wa AUSSOM, Somalia

Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limepitisha kwa kauli moja azimio la kuongeza muda wa Ujumbe wa Umoja wa Afrika wa Msaada na Kurejesha utulivu nchini Somalia (AUSSOM) kwa mwaka mmoja zaidi, hadi tarehe 31 Desemba 2026.

Akilihutubia Baraza hilo la Usalama, Naibu Mwakilishi wa Kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa, Sun Lei, amesema pengo la ufadhili linaloikabili AUSSOM kwa sasa haliwezi kuhimilika, huku upungufu wa fedha unaoikabili Ofisi ya Umoja wa Mataifa Somalia, UNSOS, ukiibua wasiwasi. Amesema China inazitaka nchi washirika wa kimataifa, hususan wafadhili wa jadi, kutimiza ahadi zao za awali na kuchukua hatua za haraka kupunguza shinikizo la kifedha linaloikabili AUSSOM.

Wakati huo huo, Ujumbe wa Umoja wa Afrika nchini Somalia (AUSSOM) umepokea kwa furaha uamuzi wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wa kuongeza muda wa jukumu lake kwa mwaka mmoja zaidi.

Balozi El Hadji Ibrahima Diene, Mwakilishi Maalumu wa Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika kwa Somalia na Mkuu wa AUSSOM, alieleza kuwa kuongeza muda huo ni uthibitisho wa imani ya Baraza katika nafasi ya Umoja wa Afrika ya kuendeleza amani, usalama na uthabiti nchini Somalia.