UN: Kutoadhibiwa wahalifu kunaeneza hisia za mauaji ya kimbari nchini Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i139298-un_kutoadhibiwa_wahalifu_kunaeneza_hisia_za_mauaji_ya_kimbari_nchini_nigeria
Ripoti ya Umoja wa Mtaifa inasema, kutoadhibiwa watu wanaofanya mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya viongozi wa kidini na sehemu za ibada, pamoja na kinga dhaifu na uwajibikaji duni, vinawafanya waathiriwa nchini Nigeria kuona kwamba vurugu zinazofanyika nchini humo ni mateso au hata mauaji ya halaiki.
(last modified 2026-06-21T02:55:21+00:00 )
Jun 21, 2026 02:52 UTC
  • Wahamga wa makundi ya waasi, Nigeria
    Wahamga wa makundi ya waasi, Nigeria

Ripoti ya Umoja wa Mtaifa inasema, kutoadhibiwa watu wanaofanya mashambulizi ya mara kwa mara dhidi ya viongozi wa kidini na sehemu za ibada, pamoja na kinga dhaifu na uwajibikaji duni, vinawafanya waathiriwa nchini Nigeria kuona kwamba vurugu zinazofanyika nchini humo ni mateso au hata mauaji ya halaiki.

Mtaalamu mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu suala hilo amesema kwamba kuenea vurugu na kutoadhibiwa makundi yenye silaha kunadhoofisha uhuru wa kidini nchini Nigeria, akiongeza kuwa inaeleweka kwamba baadhi ya waathiriwa "wanalieleza suala hili kama mateso au mauaji ya kimbari".

Maoni haya ya Ripota Maalumu wa Umoja wa Mataifa kuhusu Uhuru wa Kidini, Nazila Ghanea, yamekuja baada ya Rais wa Marekani, Donald Trump kuikera Nigeria mwaka jana kwa kulaani kile alichodai bila ushahidi kuwa ni "mauaji ya kimbari" ya Wakristo nchini humo.

Nigeria, ambayo imegawanyika kati ya kaskazini mwa nchi yenye Waislamu wengi na kusini yenye Wakristo wengi, inajitahidi kukabiliana na migogoro mingi ya kiusalama, ikiwa ni pamoja na uasi wa muda mrefu wa kundi la Boko Haram na magenge ya "majambazi" kaskazini, pamoja na migogoro ya wakulima na wafugaji.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Nigeria, Yusuf Tuggar, amepinga madai ya Rais wa Marekani Donald Trump kuhusu mauaji ya Wakristo nchini Nigeria, akionya dhidi ya kauli zinazoweza kuchochea mgawanyiko wa kidini au kikabila nchini humo.

Vilevile, Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika (AU) amekanusha vikali madai ya Rais wa Marekani, Donald Trump, kuhusu mauaji ya kimbari dhidi ya Wakristo kaskazini mwa Nigeria.

Mahmoud Ali Youssouf amesema, mtu anapaswa kufikiria kwa kina kabla ya kutoa matamko ya aina hiyo, akisisitiza kuwa waathiriwa wengi wa mashambulizi ya kundi la Boko Haram ni Waislamu na wala sio Wakristo.