Jumamosi, Julai 15, 2017
Leo ni Jumamosi tarehe 20 Mfunguo Mosi Shawwal 1438 HIjria mwafaka na tarehe 15 Julai mwaka 2017 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 621 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria aliaga dunia Majdudeen Abu Twahir Muhammad bin Yaakub Firoozabadi. Alikuwa msomi mahiri wa lugha. Alikuwa amebobea katika elimu za hadithi, tafsiri na historia na ameandika vitabu vingi katika uwanja huo. Baadhi ya vitabu mashuhuri vya Yaakub Firoozabadi ni Qamus, Safar al-Saadah na Tanwir al-Miqyas.***

Miaka 107 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, alikufa shahidi Ayatullah Sayyid Abdullah Bahbahani mwanazuoni mahiri na mmoja wa viongozi wa wapigani uhuru nchini Iran. Alizaliwa mjini Najaf Iraq na kuanza kusoma masomo ya dini kwa baba yake Sayyid Ismail Mujtahid Bahbahani. ***
Katika siku kama ya leo mfalme wa Syria aliyewekwa na Uingereza alifanikiwa kuwa mfalme wa Iraq baada ya kukimbia kutoka Damascus. Julai 15 mwaka 1920, baada ya vikosi vya Ufaransa kukaribia mji wa Damascus, Amir Feisal aliyekuwa ametawalishwa na Uingereza huko nchini Syria aliukimbia mji huo. Syria na Lebanon ni miongoni mwa ardhi zilizokuwa chini ya mamlaka ya utawala wa Othmania ambazo mwishoni mwa Vita vya Kwanza vya Dunia zikawa moja ya hisa za Ufaransa. Julai mwaka huo huo, Syria ikakaliwa kwa mabavu na vikosi vya Ufaransa. Amir Feisal ambaye aliongoza Syria miezi mitatu tu akiwa Mfalme, baadaye akatawalishwa na Uingereza na kuwa Mfalme wa Iraq. ***
Siku kama ya leo miaka 78 iliyopita inayosadifiana na tarehe 24 Tir 1318 Hijria Shamsia, alizaliwa Ayatullahil Udhma Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mji wa Mash'had ulioko kaskazini mashariki mwa Iran. Baada ya kumaliza masomo katika shule ya sekondari, alijikita zaidi katika masomo ya kidini kutoka kwa baba yake, na kupiga hatua kubwa ya kielimu katika kipindi kifupi. Ayatullah Khamenei alielekea mjini Qum kwa masomo ya juu ya kidini na kupata fursa ya kunufaika na elimu kutoka kwa maulamaa wakubwa katika mji huo, kama vile Imam Khomeini MA, Ayatullahil Udhma Burujerdi na Allamah Tabatabai katika masomo ya fiqh, usulul na falsafa. Akiwa bado kijana, Sayyid Khamenei alikuwa mstari wa mbele katika harakati za mapinduzi dhidi ya utawala kibaraka wa Shah hapa nchini, na mara kadhaa alitiwa mbaroni, kutumikia vifungo na hata kupelekwa uhamishoni. Baada ya kufariki dunia Imam Khomeini MA mwaka 1368 Hijria Shamsia, Baraza la Wanachuoni linalomchagua Kiongozi wa Mkuu wa Iran, lilimchagua Ayatullah Khamenei wakati huo akiwa rais wa nchi, kuwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu. ***
Katika siku kama ya leo miaka 73 iliyopita, tarehe 15 Julai mwaka 1944, jeshi la Marekani lilianza kuishambulia Japan kwa maelfu ya mabomu wakati wa kipindi cha Vita vya Pili vya Dunia. Mashambulio hayo ya mabomu ya Marekani yaliendelea hadi Japan iliposalimu amri. Tukio hilo chungu licha ya kusababisha makumi ya maelfu ya wananchi wasio na hatia wa Japan kuuawa kwa halaiki, lilipelekea pia zaidi ya viwanda elfu tatu vikubwa kwa vidogo kuharibiwa kabisa. ***
Siku kama ya leo miaka 59 iliyopita, Nuri Said Pasha Waziri Mkuu wa zamani wa Iraq aliuawa baada ya kujiri mapinduzi ya umwagaji damu. Alijunga na jeshi la utawala wa Othmania akiwa na umri wa miaka 21 na kushiriki katika vita vya utawala wa Othmania na Bulgaria vilivyojiri mwaka 1912. Nuri Said Pasha sambamba na kuwa mwanajeshi, alianzisha harakati za kisiasa na alizingatiwa na Uingereza wakati wa malalamiko ya kisiasa dhidi ya utawala wa Othmania. Hatimaye mwaka 1930 akipata himaya ya Uingereza alichaguliwa kuwa waziri Mkuu wa Uingereza. ***
Katika siku kama ya leo miaka 49 iliyopita, yaani tarehe 24 Tir mwaka 1347 Hijria Shamsia, Ismail Balkhi mwanamapambano na mwanafikra wa Kiafghani alikufa shahidi mjini Kabul. Alizaliwa katika kijiji kimoja kaskazini mwa Afghanistan. Alianza kusoma kwa bidii masomo ya dini tangu akiwa mdogo na kipindi fulani alifanya safari nchini Iran na Iraq, lengo likiwa ni kujiendeleza zaidi kielimu katika masomo ya dini. Ismail Balkhi alikuwa akiendesha mapambano dhidi ya udikteta na daima alikuwa akiwashajiisha wananchi Waislamu wa Afghanistan kupambana na tawala dhalimu. Kutokana na harakati hizo, shahidi Balkhi alikuwa chini ya mashinikizo ya watawala wa wakati huo wa Afghanistan, na kwa miaka kadhaa alifungwa jela. ***
Na katika siku kama ya leo miaka 7 iliyopita inayosadifiana na tarehe 24 Tir 1389 Hijria Shamsia, kwa akali watu 27 waliuawa na wengine 169 kujeruhiwa, kwenye milipuko miwili ya mabomu iliyotokea katika mji wa Zahedan, ulioko kusini mashariki mwa Iran. Milipuko hiyo ilitokea mkabala na Msikiti Mkuu wa Zahedan, wakati wa kufanyika sherehe za kuadhimisha siku ya kuzaliwa Imam Hussein bin Ali bin Abi Talib AS mmoja kati ya wajukuu wa Mtume Mtukufu Muhammad SAW. Kikundi cha kigaidi kilichojulikana kwa jina la Jundullah, ndicho kilichotekeleza shambulio hilo la kigaidi.