Jumapili, Agosti 20, 2017
Leo ni Jumapili tarehe 27 Dhulqaadah mwaka 1438 Hijria, inayosadifiana na tarehe 20 Agosti 2017 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 125 iliyopita alifariki dunia Mirza Mohammad Reza Kalhor, mchoraji maarufu wa enzi za utawala wa Qajar nchini Iran. Kolhor aliyekuwa mtoto wa Rahim Beik, alizaliwa mwaka 1245 Hijiria katika eneo la Kolhor, Kermanshah nchini Iran. Akiwa kijana mdogo alijifunza fani ya mbio za farasi na ulengaji shabaha lakini baadaye akavutiwa na uchoraji na kuanza kujifunza fani hiyo ambapo alisafiri hadi mjini Tehran kwa ajili ya kujiendeleza zaidi. Baada ya kufika mjini Tehran alianza kusomea fani hiyo ya uchoraji kwa Mirza Mohammad Khansari ambapo aliinukia haraka na kuanza kudhihirisha kipawa chake na hatimaye kupata umaarufu mkubwa katika uga huo.
Siku kama ya leo miaka 103 iliyopita, mji wa Brussels, Ubelgiji ulidhibitiwa na askari wa Ujerumani. Huo ulikuwa mji mkuu wa kwanza kudhibitiwa na askari wa Ujerumani wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Licha ya Ubelgiji kutangaza msimamo wake wa kutokuwa upande wowote katika vita hivyo, hata hivyo tarehe nne Agosti 1914 askari wa Ujerumani walianza kushambulia ngome imara ya kijeshi ya Ubelgiji huku wakiuvamia kabisa mji mkuu wa nchi hiyo Brussels sawa na siku kama ya leo mwaka huo.
Siku kama ya leo miaka 29 iliyopita, Marekani ilikubali kosa lake la kushambulia ndege ya abiria ya Iran tukio lililojiri mwezi wa Tir 1367 Hijiria Shamsia. Itakumbukwa kuwa tarehe 12 Tir mwaka 1367 Hijiria Shamsia sawa na tarehe tatu Julai 1988 Miladia, ndege ya abiria ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iliyokuwa imetokea mji wa Bandar Abbas kuelekea Dubai, na ikiwa katika anga ya maji ya Ghuba ya Uajemi na karibu na kisiwa cha Hangam, ilishambuliwa na meli ya kivita ya Marekani na kuangukia baharini. Ndege hiyo ilitunguliwa kwa makusudi na kombora la manowari ya Marekani ya Vincennes na kupelekea wasafiri 298 wakiwamo abiria na wahudumu wake kuanzia watoto, wanawake, vijana na wazee kuuawa shahidi. Aidha katika tukio hilo la kinyama, Marekani iliua watoto 66 waliokuwa na umri chini ya miaka 13, wanawake 53 na watu 46 wenye uraia wa nchi tofauti. Baada ya kupita karibu siku 45 tangu kujiri tukio hilo, serikali ya Marekani sambamba na kutangaza kuwa hujuma hiyo ilifanyika kwa bahati mbaya, ilikuwa imempatia medali ya ushujaa na heshima kamanda wa meli iliyohusika na mauaji hayo ya kinyama.
Siku kama ya leo miaka 26 iliyopita, Estonia ambayo ni miongoni mwa nchi za Baltic huko magharibi mwa Urusi ya zamani ilijitangazia uhuru. Estonia ilikuwa chini ya satwa ya Urusi ya zamani kufuatia makubaliano ya siri yaliyofikiwa mwaka 1939 Miladia kati ya Hitler na Stalin. Mwaka 1991, karibu asilimia 80 ya wananchi wa Estonia walishiriki kwenye kura ya maoni na kupelekea kutangazwa uhuru wa nchi hiyo katika siku kama hii.
Siku kama ya leo miaka miwili iliyopita, winchi moja lililokuwa limesimikwa upande wa mashariki mwa msikiti wa Makka lilianguka na kusababisha maafa kwa mahujaji wengi wa nyumba ya Mwenyezi Mungu mtukufu. Katika tukio hilo lililojiri siku ya Ijumaa ya tarehe 27 Dhul-Qaadah sawa na tarehe 11 Septemba 2015, majira ya 17:10 kwa wakati wa mji wa Makkah, mahujaji 107 waliuawa na wengine 238 walijeruhiwa. Akthari ya mahujaji waliopoteza maisha katika tukio hilo lililotajwa na walimwengu wote kuwa la uzembe, walikuwa raia wa Pakistan, Indonesia, India na Iran.