May 09, 2018 03:00 UTC
  •  Jumatano,  9 Mei,  2018

Leo ni Jumatano tarehe 22 Shaabani 1439 Hijria mwafaka na tarehe 9 Mei mwaka 2018 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 666 iliyopita Ibn Hajar Asqalani, faqih, mwanahadithi, mwanahistoria na mshairi Mwislamu wa Misri alizaliwa mjini Cairo Misri. Alimpoteza baba yake mzazi alipokuwa na umri wa miaka mitano tu na katika umri huo akaanza kujifunza Qur'ani Tukufu pamoja na masomo mengine ya kidini. Kufikia miaka 10 alikuwa amehifadhi Qur'ani nzima na alisafiri katika nchi tofauti kwa lego la kupata masomo ya juu. Alionyesha kipawa na ujuzi mkubwa katika taaluma ya hadithi kiasi kwamba lifahamika kwa jina la Hafidh Mkubwa wa Hadithi. Ibn Hajar Asqalani anahesabiwa kuwa miongoni mwa waandishi mashuhuri katika ulimwengu wa Kiislamu, kwa kadiri kwamba ameandika vitabu vinavyopata 150. Miongoni mwa vitabu hivyo ni Lisaanul Mizaan, Fat'hul Bari fii Sharh Hadithil-Bukhari na al-Ishara fii Tamyiz as-Swahaba. Ibn Hajar al-Asqalani aliaga dunia mwaka 852 Hijiria.

Ibn Hajar Asqalani 

Siku kama ya leo miaka 365 iliyopita, kazi ya ujenzi wa jengo la Taj Mahal linalohesabiwa kuwa miongoni mwa majengo ya kuvutia zaidi duniani na moja kati ya mifano bora zaidi ya usanifu majengo wa Kiislamu huko India ilimalizika baada ya miaka 22. Ujenzi wa jengo la Taj Mahal ulianza baada ya kufariki dunia mke wa Shah Jahan, mfalme wa India huko katika jimbo la Agra. Jengo hilo lilijengwa kwa kutegemea ramani iliyochorwa na msanifu majengo mashuhuri wa Iran, Issa Isfahani. Kwa upande wa nje, jengo la Taj Mahal limenakshiwa kwa ustadi kwa rangi mbalimbali huku kuta zake zikiwa zimeandikwa maandishi ya Kiarabu yenye aya za Qur'ani Tukufu. Ndani ya jengo hilo kuna makaburi mawili ya mfalme Shah Jahan na mkewe Nur Jahan.

Jengo la Taj Mahal

Miaka 102 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 9 Mei, mkataba wa kihistoria wa Sykes-Picot ulitiwa saini na wawakilishi wa Uingereza, Ufaransa na Urusi ya zamani. Hata hivyo Umoja wa Kisovieti baadaye ulijitoa kwenye makubaliano hayo baada ya mapinduzi ya Bolshevik. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, tawala za Uingereza na Ufaransa ziligawana nchi za Kiarabu zilizokuwa chini ya mamlaka ya utawala wa Kiothmania. Kwa msingi huo Iraq na Jordan zikawa chini ya udhibiti wa Uingereza huku Syria na Lebanon zikitawaliwa na Ufaransa.

Na siku kama ya leo miaka 213 iliyopita aliaga dunia mwandishi, malenga na mwandishi wa michezo ya kuigiza wa Kijerumani kwa jina la Johann Friedrich Von Schiller akiwa na umri wa miaka 46. Von Schiller alipenda sana masuala ya uandishi tangu utotoni mwake. Friedrich Von Schiller alikuwa hodari katika fasihi ya Kijerumani na anahesabiwa kuwa mmoja kati ya waandishi mahiri wa Kijerumani katika uga wa fasihi.

Johann Schiller

 

Tags