Jun 12, 2018 04:14 UTC
  • Jumanne tarehe 12 Juni, 2018

Leo ni Jumanne tarehe 27 Ramadhani 1439 Hijria sawa na Juni 12, 2018.

Siku kama ya leo miaka 879 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 27 Ramadhani 560 Hijria, alizaliwa Muhyiddin Abubakr bin Muhammad mashuhuri kwa jina la 'Ibn A'rabi' msomi na arif mkubwa wa Kiislamu huko Andalusia kusini mwa Uhispania ya leo. Alianza kujifundisha Qur'ani Tukufu, fiqh na hadithi akiwa na umri wa miaka minane katika mji wa Andalusia. Msomi huyo wa Kiislamu ameandika vitabu kadhaa vikiwemo ' Al Futuhaatul Makiyyah', 'Fusuusul Hikam' na 'al Mabadi wal Ghaayaat.' Ibn A'rabi alifariki dunia mwaka 638 huko Damascus, Syria.

Ibn A'rabi

Tarehe 12 Juni miaka 478 iliyopita nchi ya Chile iliyoko magharibi mwa Amerika ya Kusini ilitekwa na wakoloni wa Hispania. Kabla ya hapo Wahindi Wekundu wa Chile walikuwa wamevunja hujuma na mashambulio kadhaa ya Wahispania waliokusudia kuteka na kukalia kwa mabavu ardhi yao. Hata hivyo, hata baada ya kutekwa nchi yao, Wahindi Wekundu hao waliendeleza mapambano dhidi ya wakoloni hadi pale José Francisco de San Martín jenerali wa Argentina alipowasili mwaka 1817 na kuanzisha mashambulio ya kuzikomboa nchi zote zilizokuwa chini ya ukoloni wa Hispania Kusini mwa Amerika, ikiwemo Chile. Kwa msingi huo, Chile akakombolewa na kutangaza uhuru wake mwaka 1818.

Bendera ya Chile

Siku kama ya leo miaka 329 iliyopita alifariki dunia Allamah Muhammad Baqir Majlisi, mmoja kati ya maulamaa wakubwa wa Kiislamu. Baba yake Allamah Majlisi alipata elimu kwa msomi mkubwa wa Kiislamu Sheikh Bahai. Umahiri wa Sheikh Majlisi ulianza kuonekana akiwa bado kijana na alipata ijaza au ruhusa ya kunukuu hadithi kutoka kwa msomi na mwanafalsafa mashuhuri wa Kiislamu Mulla Sadra akiwa na umri wa miaka 14 tu. Allamah Majlisi ameandika vitabu vingi wakati wa uhai wake ambavyo hii leo ni marejeo ya Waislamu. Katika kipindi cha uhai wake Allamah Muhammad Baqir Majlisi alifanya hima kubwa kuhakikisha kuwa Swala za Ijumaa na jamaa zinatekelezwa. Vilevile alifanya juhudi za kuasisi shule za masomo ya kidini na kueneza hadithi za Mtume wa Muhammad (saw) na Ahlubaiti zake watoharifu. Idadi ya vitabu vilivyoandika na Allamah Muhammad Baqir Majlisi imetajwa kuwa zaidi ya 600 na mashuhuri zaidi ni kile kinachojulikana kwa jina la Biharul Anwar. Vitabu vingine mashuhuri vya msomi huyo ni Hayatul Quluub, Ainul Hayaat na Zadul Maad.

Allamah Muhammad Baqir

Tarehe 12 Juni 1914, kwa mara ya kwanza kabisa yalifanyika majaribio ya kutumia nishati ya joto la jua pambizoni mwa Cairo mji mkuu wa Misri. Mbunifu na mtekelezaji wa mpango huo alikuwa mwanafizikia wa Kijerumani, ambaye aliweza kukusanya miale ya jua na kufanikiwa kuwasha mashine ya mvuke yenye kutumia 'horse power' 50.

Nishati ya Jua

Siku kama ya leo miaka 54 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 12 Juni 1964, Nelson Mandela kiongozi wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini alihukumiwa kifungo cha maisha jela, baada ya kupatikana na hatia ya kufanya uhaini dhidi ya mfumo na utawala wa ubaguzi wa rangi, Apartheid nchini humo. Mandela alihukumiwa adhabu hiyo pamoja na wenzake saba akiwemo Walter Sisulu aliyekuwa Katibu Mkuu wa zamani wa chama cha African National Congress kilichokuwa kimepigwa marufuku nchini humo. 

Image Caption

Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita inayosadifiana na tarehe 12 Juni 1975, Indira Gandhi Waziri Mkuu wa wakati huo wa India alizuiwa kuendelea na wadhifa huo kwa miaka sita, baada ya kupatikana na hatia ya kufanya udanganyifu katika uchaguzi. Hata hivyo Indira Gandhi alipinga miito iliyomtaka ajiuzulu na akatangaza mipango ya kukata rufaa katika mahakama kuu ya India. Siku kama ya leo miaka 470 iliyopita, ardhi ya Chile huko magharibi mwa Amerika ya Kusini ilivamiwa na wakoloni wa Kihispania. Kabla ya uvamizi huo, Wahindi Wekundu wa Chile waliushinda uvamizi wa Uhispania uliokuwa na lengo la kuikalia kwa mabavu ardhi yao. 

Indira Gandhi

Siku kama ya leo miaka 27 iliyopita inayosadifiana na 12 Juni 1991, ulifanyika uchaguzi wa kwanza wa Rais wa Shirikisho la Russia. Baada ya kusambaratika Urusi ya zamani, Russia kama zilivyokuwa nchi nyingine zilizokuwa zikiunda Umoja wa Kisovieti zilijipatia uhuru wake. Boris Yeltsin aliiongoza nchi hiyo kwa vipindi viwili, hadi mwezi Disemba 1999, alipoamua kung'atuka madarakani.

Bendera ya Russia