Jun 14, 2018 02:20 UTC
  • Alkhamisi, Juni 14, 2018

Leo ni tarehe 29 Ramadhani 1439 Hijria sawa na Juni 14, 2018.

Tarehe 29 Ramadhani miaka 791 iliyopita alizaliwa Jamaluddin Hassan bin Yusuf aliyepea laqabu ya Allamah Hilli, alimu, mtaalamu wa hadithi na mwanafasihi mkubwa wa Kiislamu. Awali Jamaluddin alisoma elimu mbalimbali kama fiq’hi, usulul fiq’hi na hadithi kwa baba yake na kufikia daraja za juu katika nyanja hizo. Msomi huyo mkubwa ameandika vitabu vingi vya thamani kama “Tadhkiratul-Fuqahaa”, “Irshaadul-Adh’haan" na "Kashful Murad.”

Allamah Hilli

Siku kama ya leo miaka 632 iliyopita, alifariki dunia Ibn Furat, faqih, mwanahistoria na mhadhiri wa nchini Misri. Ibn Furat alizaliwa mjini Cairo mwaka 735 Hijiria na kuanza masomo yake akiwa kijana mdogo. Msomi huyo alijikita sana katika masuala ya historia, kiasi cha kumfanya aandike vitabu mbalimbali katika uwanja huo. Miongoni mwa athari muhimu za Ibn Furat ni pamoja na kitabu kiitwacho ‘Taarikhud-Duwal wal-Muluuk’, kitabu ambacho kina historia na matukio ya karne ya sita Hijria.

Siku kama ya leo miaka 282 iliyopita alizaliwa mwanafikizia wa Kifaransa kwa jina la Charles-Augustin de Coulomb. Msomi huyo alianza kufundisha masomo katika taaluma ya umeme na sumaku baada ya kuhitimu masomo yake na kuandika vitabu vingi katika uwanja huo. Mbali na kufundisha, mwanafizikia Augustin de Coulomb aliendelea kufanya utafiti na hatimaye akafanikiwa kubuni kanuni katika sayansi ya fizikia iliyojulikana kwa jina Lake. De Coulomb aliaga dunia akiwa na umri wa miaka 70.

Charles-Augustin de Coulomb

Siku kama ya leo miaka 198 iliyopita, wanajeshi wa Misri wakiongozwa na Kamanda Muhammad Ali Pasha waliishambulia Sudan na kulikalia kwa mabavu eneo kubwa la ardhi ya kaskazini mwa nchi hiyo. Wakati huo huo Waingereza pia walilishambulia eneo la kusini mwa Sudan na kulikalia kwa mabavu. Hata hivyo mwaka 1881 wananchi wa Sudan wakiongozwa na Mahdi Sudani walianzisha harakati ya ukombozi dhidi ya uvamizi wa Misri na Uingereza na mwaka 1885 wakafanikiwa kutoa pigo kubwa kwa vikosi vamizi vya Misri na Uingereza na kukomboa eneo kubwa la nchi yao.

Sudan

Siku kama ya leo miaka 188 iliyopita, wanajeshi wa Ufaransa waliwasili katika pwani ya Algeria huko kaskazini mwa Afrika. Uvamizi huo ulikuwa mwanzo wa oparesheni za kijeshi za Ufaransa zilizokuwa na lengo la kuikalia kwa mabavu na kuikoloni Algeria. Hata hivyo uvamizi huo wa kikoloni ulikabiliwa na mapambano makubwa ya wananchi dhidi ya maghasibu wa Kifaransa. Mapambano hayo ya kupigania ukombozi ya wananchi wa Algeria dhidi ya ukoloni wa Ufaransa yalipamba moto baada ya kumalizika Vita vya Pili vya Dunia. Hatimaye mwaka 1962 rais wa wakati huo wa Ufaransa alilazimika kuipatia Algeria uhuru kamili, kufuatia mashinikizo ya mapambano ya wananchi wa Algeria na upinzani wa fikra za walio wengi ndani ya Ufaransa kwenyewe na kimataifa.

Bendera ya Algeria

Tarehe 24 Khordad miaka 37 iliyopita wabunge 120 wa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu waliwasilisha muswada wa kutokuwa na imani na Rais wa wakati huo Bani Sadr. Kwa utaratibu huo kiongozi huyo alilazimika kung'atuka madarakani. Bani Sadr ni miongoni mwa watu waliojidhihirisha kuwa wapenzi na watetezi wa harakati za Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran baada ya Imam Khomeini kuhamia Paris, Ufaransa na alifanikiwa kushika madaraka ya nchi na kuwa rais katika uchaguzi wa kwanza wa baada ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini kwa kutumia ujanja wa kipropaganda. Muda mfupi baadaye Imam Khomeini alimkabidhi ukamanda wa majeshi ya Jamhuri ya Kiislamu. Hata hivyo Bani Sadr aliyekuwa mtu mwenye uchu wa madaraka, mwenye kiburi na msaliti alianza mara moja kushirikiana na makundi yaliyokuwa yakipinga Mapinduzi ya Kiislamu kwa lengo la kuangusha utawala wa Kiislamu nchini Iran. 

Bani Sadr

Na siku kama ya leo miaka 32 iliyopita, alifariki dunia Jorge Luis Borges, mwandishi mkubwa wa Amerika ya Latini. Luis alizaliwa mwaka 1899 Miladia nchini Argentina na kutokana na kutalii sana athari za wasomi wakubwa kama vile Edgar Allan Poe, Charles Dickens na Cervantes akafanikiwa kuinukia na kuwa hodari katika uwanja huo. Mwishoni mwa masomo yake, Jorge Luis Borges akaanza shughuli ya uandishi na taratibu akaanza kuandika kisa mashuhuri cha Amerika ya Latini. Hata hivyo kutokana na upofu wake, hakuweza kumaliza kuandika kisa hicho. Luis ameacha athari mbalimbali za vitabu ambavyo vinapatikana katika maktaba mbalimbali za dunia.

Jorge Luis Borges