Jun 22, 2022 06:33 UTC
  • Hassanain katika Aya ya Tat'hir 1

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na karibuni kusikiliza sehemu ya tano ya mfululizo wa vipindi hivi vya Sibtain katika Qur'ani na Jadithi. Sibtain ni Imam Hassan na Imam Hussein (as) ambao ni wajukuu wa Mtume Mtukufu (saw), kati ya wema wa Ahlul Bait (as) ambao kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu yaliyojaa rehema na hekima, aliwajaalia kuwa watu bora zaidi katika jamii ya wanadamu kwa kusema: Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni u

Na Aya hii ndugu wasikilizaji, ni uthibitisho, ushihidi na waraka wa Mwenyezi Mungu unaothibitisha nafasi aali na ya juu kabisa waliyonayo Ahlu Beit wa Mtume (saw) mbele ya Mungu Muumba, nao ni Muhammad al-Mustafa, Ali al-Murtadha, Swadiqatul Kubra Fatwimat az-Zahra, Al-Hassan na al-Hussein (as) ambao ni mabwana wa mabarobaro wa Peponi. Aya hii kama wanavyosema waandishi wa vitabu vya Swihah, inabainisha dua ya Mtume (saw) kwa Ahlul Bait wake baada ya kuwakarimu kwa kuwafunika kwa shuka lake takatifu (kisaa) kisha akawaombea kwa kusema: 'Ewe Mwenyezi Mungu hawa ndio Ahlu Bait wangu, hivyo waondolee uchafu na uwatakase baarabara.'

Na Riwaya zilizopokelewa kuhusiana na Aya hii takatifu Wapenzi wasikilizaji, ni miongoni mwa Riwaya zilizopokelewa na kunukuliwa kwa wingi zaidi kuhusiana na watakatifu hawa watano wa Ahlu Kisaa. Kwa kadiri kwamba ni nadra kupata kitabu chochote cha tafsiri au Hadithi, historia ya Kiislamu au inayohusiana na maisha ya Mtume (saw), ambacho hakijazungumzia Riwaya na Aya ya Tat'hir inayozungumzia watukufu hawa (as). Inatosha kujua kwamba al-Hafidh al-Haskani, ambaye ni msomi wa Kihanafi amekusanya katika kitabu chake cha Shawahid at-Tanzil Liqawaid at-Tafdhil Hadithi 188 zinazozungumzia Aya hii ya Tat'hir kama ambavyo mfasiri mkubwa wa Qur'ani na mtafiti Sayyid Hashim al-Bahrani amekusanya katika kitabu chake cha Ghayatul Maram, Hadithi 41 kutoka vitabu vya Ahlu Sunna bila kujumuisha vitabu vya Shia, zinazohusiana na Aya hii. Ni wazi kuwa baada ya kuzungumzia suala hili, tunasubiri kwa hamu kujua sababu ya kuteremka Aya takatifu ya Tat'hir. Tutalijadili suala hilo hivi punde, hivyo endeleeni kuwa nasi.

***********

Ndugu wasikilizaji, vitabu vya historia vinatwambia kwamba Mtume aliporejea kutoka katika medani ya vita, kaskazini mashariki mwa mji wa Madina, yaani Khaibar, Wadi al-Qura na Fadak na baada ya kuwa hali ilikuwa imetulia huko, siku moja mapema asubuhi alikuwa nyumbani kwa Umul Mu'mineen, Ummu Salama ambapo alitazama mbinguni na hapo rehema ya Mwenyezi Mungu akiwa imeteremka. Akiwa katika hali hiyo, binti yake Fatwimah az-Zahra (as) alifika mbele yake na akamuuliza: "Je, yuko wapi mwana wa ami yako? Akamjibu (Fatwimah): Yuko nyumbani. Mtume (saw) akamwambia: Nenda ukamwite na uje na wanawe wawili. Kisha akarejea kwake Mtume (saw) huku akiwa ameandamana na wanawe wawili al-Hassan na al-Hussein ambao katika kipindi hicho walikuwa wangali wadogo, na Ali ambaye alikuwa akiwafuata nyuma. Mtume akamwambia Ummu Salama: Simama uwaondokee Ahlu Bait wangu. Ummu Salama akawa ameondokea na kuelekea mlangoni. Mtume (saw) akamchukua al-Hassan na al-Hussein na kuwapeleka chumbani kwake na akawa anawabusu. Akamkumbatia Ali kwa mkono wake mmoja na Fatwimah kwa mkono wake wa pili na kuwabusu. Ali akawa ameketi upande wake wa kulia naye Fatwimah upande wake wa kushoto. Kisha Mtume akawafunika kwa shuka lake na kusema: 'Ewe Mwenyezi Mungu hawa ni Aali wa Muhammad, hivyo jaalia swala na baraka zako ziwe juu ya Muhammad na Aali Muhammad, hakika wewe ni mwenye kuhimidiwa na mtukufu. Allahuma! Hawa ni Ahlu Bait wangu ambao uliniahidi kwao kile ulichoniahidi. Kisha alifungua upande mmoja wa Kisaa (shuka) na kunyanyua juu mkono wake mtukufu na kusema: 'Allahuma! Hakika kila Nabii ana ahli zake na hawa ndio Ahlu Bait wangu, wanaohusiana nami moja kwa moja, na nyama yangu.  Kinaniuma kinachowauma wao na kinanijeruhi kinachowajeruhi wao. Hivyo, waondolee uchafu na uwatakase kabisa kabisa. Kisha akasema: 'Allahuma! Hawa ni Ahli zangu, nitampiga vita kila anayewapiga vita, kuwa salama kwa wale wanaokuwa salama kwao, kuwapenda wanaowapenda na kumchukia kila anayewachukia. Hivyo mpige vita kila anayewapiga vita, kuwa salama kwa anayekuwa salama kwao, mpende anayewapenda na mchukie anayewachukia."

********

Ndugu wasikilizaji, tunaendelea kujadili kisa cha Ahlu Kisaa na Aya ya Tat'hir ambapo tunakiunganisha kisa hicho hapa na Riwaya iliyopokelewa kutoka kwa Ibn Abbas ambaye anasema kuwa Mtume Mtukufu (saw) amesema: 'Hakika Ali ni Wasii na Khalifa wangu, na mke wake, Fatwima, mbora wa wanawake wa Peponi ni binti yangu, na Hassan na Hussein, mabwana wa mabarobaro wa Peponi ni wana wangu. Kila anayewapenda huwa amenipenda mimi na anayewafanyia uadui huwa amenifanyia mimi uadui, kila anayejiweka mbali nao huwa amejiweka mbali nami, kuwatenga wao ni kunitenga mimi na kuwatendea wema ni kunitendea wema mimi. Mwenyezi Mungu hujiunga na kila anayejiunga nao na hukata uhusiano na kila anayekata uhusiano nao, huwasaidia wanaowasaidia na kuwadhalilisha wanaowadhalilisha. Allahuma! Kila mmoja wa Manabii wako alikuwa na Aali zake; hivyo Ali, Fatwima, Hassan na Hussein (as) ni Ahli na Watu wa Nyumba yangu. Waondolee uchafu wote na uwatakase kabisa kabisa."

Akasema: Hapo Malaika Jibril al-Amin akateremka akiwa amebeba Wahyi huku akiwa ameandamana na Malakika Mikail ambao wote kwa pamoja walimsomea Aya inayofuata: Hakika Mwenyezi Mungu anataka kukuondoleeni uchafu, enyi Watu wa Nyumba ya Mtume, na kukutakaseni baarabara.

Mtume akamgeukia Ali na kumwambia: Ewe Ali! Aya hii imeteremka kukuhusu wewe, Hassan na Hussein pamoja na Maimamu wa kizazi chako. Ali akasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Ni Maimamu wangapi watakaokuja baada yako? Mtume (saw) akajibu: Wewe Ali, kisha watoto wako wawili, Hassan na Hussein na kisha baada ya Hussein ni mwanae Ali, baada ya Ali ni mwanae Muhammad, baada ya Muhamad ni mwanae Ja'ffar, baada ya Ja'ffar ni mwanae Musa, baada ya Musa ni mwanae Ali, baada ya Ali ni mwanae Muhammad, baada ya Muhammad ni mwanae Ali, baada ya Ali ni mwanae Hassan na baada ya Hassan ni mwanae al-Hujja (Imam wa zama (af)). Hivi ndivyo nilivyopata majina hayo yakiwa yameandikwa kwenye upande wa Arshi. Nilimuuliza Mwenyezi Mungu Mtukufu sababu ya jambo hilo Naye akaniambia: Ewe Muhammad! Hao ni Maimamu baada yako. Wao ni watoharifu na maasumina na maadui wao wamelaaniwa.

Hapo Ummu Salama alitaka kuingia kwenye Kisaa lakini Mtume (saw) akamzuia na kumwambia: Usiingie humu lakini hata hivyo, uko kwenye heri. Kisha alisema kuhusiana na wapendwa wake Ali, Fatwima na Hassan na Hussein: Allahuma! Hawa ni Ahlu Bait wangu na Ahlu Bait wangu wana haki zaidi."

*********

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Sibtain katika Qur'ani na Hadithi ambapo tunatumai kimekunufaisheni vya kutosha. Basi hadi tutakapokutana tena juma linalokuja panapo majaliwa yake Mwenyezi Mungu, Tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalamma Alaykum Warahmatullahi Wabarakatuh.