Somalia yalaani shambulio la mauaji katika jimbo la Zamfara, Nigeria
-
Zamfara, Nigeria
Somalia leo imelaani vikali shambulio la umwagaji damu katika jimbo la Zamfara kaskazini magharibi mwa Nigeria lililouwa raia wasiopungua 50. Wanawake na watoto pia walitekwa nyara katika hujuma hiyo ya kigaidi.
Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Somalia imesema, nchi hiyo iko pamoja na bega kwa bega na serikali na wananchi wa Nigeria na imetoa pole kwa familia za wahanga.
Mogadishu imetoa wito wa kuachiwa huru mateka wote bila ya masharti na kuunga mkono jitihada za serikali ya Nigeria za kuwafikisha mbele ya vyombo vya sheria wahusika wa jinai hiyo.
"Afrika inapasa kuungana na kupambana dhidi ya ugaidi na kuwalinda raia,' imeeleza taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Somalia.
Shambulio lililofanywa na makundi ya wanamgambo waliokuwa na silaha wanaotajwa kama majambazi yalianza usiku wa Alhamisi iliyopita na kuendelea hadi Ijumaa asubuhi.
Majambazi hao waliokuwa kwenye pikipiki walichoma moto nyumba kadhaa na kuwapiga risasi wenyeji wa kijiji cha Tungan Dutse wakati walipokuwa wakijaribu kuwahepa wahalifu hao.
Nigeria imeathiriwa na ukosefu wa usalama, hali ambayo inaongezeka kila uchao hususan upande wa kaskazini magharibi mwa nchi hiyo, eneo lilipo jimbo la Zamfara. Eneo hilo limekuwa likikumbwa na mashambulizi ya majambazi, utekaji nyara na mauaji na kulazimisha maelfu ya watu kuyahama makazi yao.