May 20, 2023 02:14 UTC
  • Jumamosi, 20 Mei, 2023

Leo ni Jumamosi tarehe 29 Mfunguo Mosi Shawwal 1444 Hijria mwafaka na tarehe 20 Mei, 2023 Miladiia.

Miaka 517 iliyopita katika siku kama ya leo, yaani tarehe 20 Mei mwaka 1506 aliaga dunia baharia mashuhuri wa Kiitalia Christopher Columbus. Columbus alizaliwa Septemba 21 mwaka1 451 huko kusini mwa Italia. Mwezi Agosti mwaka 1492 Christopher Columbus alianza safari yake kuelekea Bahari ya Atlantiki. Watu wengi wanamtambua Columbus kuwa mtu wa kwanza kutoka Ulaya aliyevumbua bara la America. Tangu wakati huo historia ya bara hilo iliandikwa kwa mujibu wa matakwa ya wazungu na wahamiaji wapya. Historia hiyo iliambatana na machungu ya ukoloni kutoka maeneo tofauti ya dunia dhidi ya wakazi asili wa ardhi hiyo, huku ubaguzi ukiwa mhimili wa siasa kuu iliyotekelezwa na wahamiaji wazungu. ***

Christopher Columbus.

 

Siku kama ya leo miaka 217 iliyopita alizaliwa John Stuart Mill mwanafalsafa na mwanauchumi wa Uingereza. Stuart Mill alilelewa na kufunzwa na baba yake elimu za mantiki na uchumi na baadaye kuanza kuandika magazeti. Mill pia alichaguliwa kuwa mwakilishi wa bunge la Uingereza kwa duru moja. Vitabu muhimu vya mwanauchumi huyo wa Kiingereza John Stuart Mill ni vile alivyoviita "Principals of Political Economy" na "Principals of Political Science". Mill aliaga dunia mwaka 1873. ***

John Stuart Mill

 

Katika siku kama hii ya leo miaka 121 iliyopita Cuba ilitangazwa kama jamhuri huru na wanajeshi wote wa Marekani wakaondoka katika ardhi ya nchi hiyo. Cuba ambayo iligunduliwa na Christopher Columbus tangu mwaka 1492, ilikuwa koloni la Uhispania hadi kufikia mwaka 1898 Miladia. Lakini Marekani iliingiza vikosi vyake nchini humo na kuchukua nafasi ya mkoloni Uhispania baada ya kutoa pigo na kuifukuza nchi hiyo huko Cuba, kwa kisingizio eti cha kuwaunga mkono wanamapambano wapigania uhuru wa Cuba. ***

 

Siku kama ya leo miaka 89 iliyopita Yemen ilishindwa mwishoni mwa vita vilivyojiri kati yake na Saudi Arabia baada ya nchi mbili hizo kuhitilafiana juu ya suala la mpaka na kupelekea kusainiwa makubaliano ya Ta'if kati ya Imam Yahya wa Yemen na Mfalme Abdulaziz wa Saudi Arabia. Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Yemen iliikabidhi Saudia maeneo ya Najran, Jizan na Asir kwa muda wa miaka 40. Saudia ilianzisha vita vipya dhidi ya Yemen mwezi April 2015 kwa ajili ya kuyadhibiti zaidi maeneo hayo. ***

Bendera ya Yemen

 

Miaka 63 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya Kiafrika ya Cameroon ilijipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa. Kwa miaka mingi nchi hiyo ilikuwa chini ya ukoloni wa nchi za Ulaya ikiwemo Ujerumani ambayo iliikalia kwa mabavu Cameroon kuanzia mwaka 1884.  Baada ya Ujerumani kushindwa katika Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia Ufaransa na Uingereza ziligawana baina yao ardhi ya Cameroon. Hata hivyo haukupita muda kabla ya kuanza mapambano ya kupigania uhuru nchini humo. Hatimaye mapambano ya kupigania uhuru nchini Cameroon yalizaa matunda katika siku kama ya leo baada ya nchi hiyo iliyoko magharibi mwa Afrika kujipatia uhuru. ***

Bendera ya Cameroon

 

Siku kama ya leo miaka 60 iliyopita, mwafaka na tarehe 20 Mei mwaka 1963, kongamano la kihistoria la nchi za Afrika lilifanyika huko Addis Ababa, Ethiopia. Madola mengi ya Kiafrika yalijinyakulia uhuru katika miaka ya 60 na 70, na katika kipindi hicho hayakuwa na uhusiano baina yao. Ili kuunda jumuiya ya kwanza iliyokusudiwa kuzikurubisha pamoja nchi za Afrika, kongamano la kwanza la nchi hizo lilifanyika katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa tarehe kama ya leo. Kongamano hilo ilikuwa hatua ya kwanza ya kuasisiwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika, OAU. Ni vyema kuashiria hapa kwamba, Umoja wa Afrika (AU) ulichukua nafasi ya Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU) ambao uliundwa mwaka 1963 kwa shabaha ya kusimamia maslahi ya nchi wanachama, kuhamasisha maendeleo ya bara hilo na kutatua migogoro kati ya nchi Afrika. ***

Umoja wa Afrika

 

Katika siku kama ya leo miaka 41 iliyopita yaani tarehe 30 Ordibehesht mwaka 1361 Hijria Shamshia, marhumu Ayatullah Akbar Hashemi Rafsanjani mmoja wa shakhsia muhimu wa Mapinduzi ya Kiislamu na Spika wa Bunge la Iran wakati huo, alitoa pendekezo la kuundwa Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Azad. Awali fikra hiyo ilitolewa katika Jumuiya ya Kiislamu ya Vyuo Vikuu. Baadaye pendekezo hilo liliwasilishwa kwa Imam Khomeini, Muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambaye aliliunga mkono na kutoa kiwango fulani cha fedha kama msaada kwa Chuo Kikuu hicho. Hii leo Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Azad ndicho Chuo Kikuu kikubwa zaidi kisicho cha kiserikali nchini Iran. ***

 Ayatullah Akbar Hashemi Rafsanjani