Oct 20, 2025 02:37 UTC
  • Jumatatu, tarehe 20 Oktoba, 2025

Leo ni Jumatatu tarehe 27 Rabiu Thani 1447 Hijria sawa na Oktoba 20 mwaka 2025.

Miaka 1093 iliyopita katika siku kama ya leo, aliaga dunia Ibn Miqsam, mpokezi wa Hadithi na mwanafasihi wa Kiislamu.

Alizaliwa huko Baghdad na alifunzwa na maulamaa wakubwa wa mji huo kama Abbas bin Fadhl Razi. Ibn Miqsam aliandika vitabu katika uwanja wa elimu ya sintaksia lakini alijikita zaidi katika elimu ya Qur'ani.

Moja ya athari za mwandishi huyo wa Kiislamu ni kitabu alichokipa jina la " Al Anwar fi Tafsiril- Qur'an.   

Siku kama ya leo miaka 198 iliyopita, inayosadifiana na 20 Oktoba 1827 kulitokea vita vya majini katika ghuba ndogo ya Navarone iliyoko kaskazini mwa bahari ya Mediteranean.

Kwenye vita hivyo, majeshi ya Uingereza, Russia na Ufaransa ambayo yalikuwa yakiiunga mkono Ugiriki, yakitumia meli za kivita, yalishambulia meli za dola ya Othmania.

Nchi hizo tatu za Ulaya ziliangamiza kabisa meli 60 za kivita za dola la Othmania na kuwateka nyara wanajeshi elfu sita. 

Siku kama ya leo miaka 166 iliyopita, alizaliwa John Dewey, msomi na mwandishi mashuhuri wa Marekani.

Dewey alikuwa amebobea mno katika elimu ya malezi na aliweza kujifunza mengi alipokuwa katika chuo kikuu cha Colombia. John Dewey alifanikiwa kuandika vitabu vingi kuhusiana na malezi na makuzi ya mtoto.

Miongoni mwa vitabu mashuhuri vya msomi huyo ni pamoja na "How we Think", "The Public and its Problems" na "Freedom and Culture". John Dewey alifariki dunia mwaka 1962 akiwa na umri wa miaka 92.   

John Dewey

Miaka 73 iliyopita mwafaka na siku kama hii ya leo, Jomo Kenyatta mwanaharakati, mwanasiasa na mpigania uhuru mashuhuri barani Afrika na Rais wa Kwanza wa Kenya alitiwa mbaroni kufuatia amri ya utawala wa kikoloni nchini Kenya.

Mzee Kenyatta alikuwa miongoni mwa watu 100 mashuhuri nchini humo waliotiwa mbaroni katika kipindi cha masaa 24 ikiwa ni katika fremu ya mpango wa kuibana Mau Mau, kundi la wapiganaji wa Kenya waliokuwa wakiupinga utawala wa kikoloni wa Waingereza.

Wakenya huadhimisha siku hii kama Sikukuu ya Mashujaa na kuwakumbuka wale wote waliopigania uhuru wa taifa hilo.   ***

Katika siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Ahmad Khansari, faqihi na marjaa mkubwa wa Kiislamu.

Akiwa na umri wa miaka 20, Ayatullah Ahmad Khansari alielekea mjini Najaf, Iraq na kustafidi na elimu kutoka kwa wasomi wakubwa kama vile Muhaqqiq Khorasani, Sayyid Muhammad Kadhim Yazdi, Shariat Isfahani na Muhaqqiq Naaini.

Alishirikiana bega kwa bega na wanazuoni wa Kiislamu wakiongozwa na hayati Imam Ruhullah Khomeini katika harakati za Mapinduzi ya Kiislamu dhidi ya utawala muovu wa Shah. Msomi huyo amelea ma lufunza wasomi wakubwa kama Ayatullah Murtadha Mutahhari, Imam Musa Sadr na Sayyid Ridha Sadr.

Mwaka 1370 Hijiria, Ayatullah Ahmad Khansari alielekea Tehran na kuwa imamu wa Swala ya jamaa katika msikiti maarufu wa ‘Sayyid Azizullah’. Ameandika vitabu vingi katika taaluma za sheria na teolojia ya Kiislamu. 

Ayatullah Sayyid Ahmad Khansari

Siku kama ya leo miaka 14 iliyopita, kiongozi wa zamani wa Libya, Kanali Muammar Gaddafi alikamatwa na wanamapinduzi karibu na mji wa bandari wa Sirte kaskazini mwa nchi hiyo na kuuawa.

Gaddafi aliuawa baada ya miezi kadhaa ya mapigano na wanamapinduzi ambapo jeshi lake liliwaua maelfu ya wananchi hususan katika miji ya Benghazi na Tripoli.

Gaddafi ambaye aliitawala Libya kwa zaidi ya miaka 42 alizaliwa mwaka 1942. Aliingia madarakani mwaka 1969 kupitia mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa madarakani mfalme Mohammad Idris al-Sanusi.   

Muammar Gaddafi