Ijumaa, tarehe 16 Juni, 2023
Leo ni Ijumaa tarehe 27 Dhulqaada 1444 Hijria sawa na tarehe 16 Juni 2023
Katika siku kama ya leo miaka 79 iliyopita, yaani sawa na tarehe 16 Juni mwaka 1944, wanajeshi wa majini wa Marekani waliaza kushambulia kwa mabomu miji ya Japan sambamba na kuulenga mji wa Fokula ulioko kusini mwa nchi hiyo. Hayo yalijiri wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Aidha mashambulizi hayo yalifanyika kwa lengo la kuilazimisha Tokyo isalimu amri. Katika mashambulizi hayo makumi ya maelfu ya raia wa Japan waliuawa na kujeruhiwa, sambamba na kuangamizwa viwanda na mashamba ya nchi hiyo. Vita hivyo vilipelekea Marekani kushambulia kwa mabomu ya nyuklia miji miwili ya Japan ya Hiroshima na Nagasaki mwezi Oktoba mwaka 1945.

Siku kama ya leo miaka 60 iliyopita sawa na tarehe 16 Juni 1963, Valentina Tereshkova mwanamke wa kwanza duniani mwanaanga kutoka Russia, alianza safari yake ya angani kwa kutumia safina ya anga iliyoitwa Vostok-6. Mwanake huyo alitua katika orbiti ya ardhi wakati ambao Valery Bykovsky mwanaanga mwingine wa Russia alipokuwa akijishughulisha pia kuzunguka dunia. Safari ya Tereshkova katika anga za juu ilifanyika miaka miwili baada ya safari ya Yuri Gagarin ambayo ilikuwa ya kwanza kufanywa na mwanadamu katika anga hizo. Katika muda wa masaa 70 na dakika 50 aliyokuwa katika anga za juu, Tereshkova alizunguka dunia mara 48.

Siku kama ya leo miaka 47 iliyopita wananchi wa Soweto huko Afrika Kusini walianza harakati za mapambano dhidi ya utawala wa ubaguzi wa rangi wa makuburu. Katika kipindi hicho Afrika Kusini ilikuwa ikitawaliwa na wazungu wachache waliodhibiti kila kitu na sheria zilizokuwa dhidi ya binadamu. Juni 16 mwaka 1976 maelfu ya wanafunzi wazalendo walifanya maandamano makubwa kupinga sera za kibaguzi katika sekta ya elimu ambayo yalikabiliwa na ukandamizaji mkubwa wa utawala wa kibaguzi. Mamia ya raia waliuawa na wengine kujeruhiwa.

Siku kama ya leo miaka 16 iliyopita, alifariki dunia Ayatullahil-udhma Sheikh Muhammad Fadhil Lankarani alimu na marjaa mkubwa wa Kiislamu baada ya kuugua. Allamah Fadhil Lankarani alizaliwa mnamo mwaka 1310 Hijria Shamsia katika mji wa kidini wa Qum huko kusini mwa Tehran na kuanza kujifunza masomo ya dini akiwa kijana mdogo. Aidha alipata kustafidi na mafunzo ya walimu wakubwa wa zama zake kama vile Ayatullahil udhma Burujerdi na Imam Khomeini Mwenyezi Mungu awarehemu. Ayatullahil Udhma Sheikh Muhammad Fadhil Lankarani katika kipindi kifupi aliweza kufikia daraja ya ijtihad.

Na miaka 8 iliyopita katika siku kama ya leo yaani 27 Dhulqaada mwaka 1436 Hijria Qamaria winchi kubwa ya ujenzi ilianguka katika eneo moja la Msikiti Mtakatifu wa Makka na kuua idadi kubwa ya mahujaji wa Baitullah al-Haram yaani Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu. Tukio hilo lilijiri Ijumaa saa 17:10 alasiri Septemba 11 mwaka 2015 ambapo winchi hiyo ilipelekea watu 107 kupoteza maisha na wengine 238 kujeruhiwa. Aghalabu ya waliopoteza maisha walikuwa ni mahujaji kutoka nchi za India, Pakistan, Indonesia na Iran. Wakuu wa Saudia walisema winchi hiyo ilianguka kutokana na upepo mkali. Tukio hilo la kusikitisha lilionyesha uzembe wa hali ya juu wa utawala wa Saudia. Tukio hilo la kuanguka winchi na maafa ya Mina wakati wa Sikukuu ya Idul Adha mwaka huo huo ni kati ya matukio machungu zaidi yaliyoshuhudiwa katika ibada ya Hija.
