Kuendelea mashinikizo ya kieneo dhidi ya utawala wa kijeshi nchini Niger
Sambamba na kuendelea kuwa madarakani utawala wa kijeshi nchini Niger, vitisho vya taasisi za kikanda vya kuongeza mashinikizo kwa nchi hiyo hususan watawala wa kijeshi vya kumrejesha madarakani rais aliyepinduliwa Muhammad Bazoum, nayo yameshadidi na kuchukua wigo mpana zaidi.
Kuhusiana na hilo, Kamisheni ya Amani na Usalama ya Umoja wa Afrika imesimamisha uanachama wa Niger katika umoja huo.
Umoja wa Afrika umetoa wito kwa nchi wanachama kujiepusha na kitendo chochote kitakachohalalisha baraza la kijeshi la Niger. Umoja huo pia ulitangaza kuwa unachunguza hatua ya Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) kuingilia kijeshi nchini Niger.
Majenerali wa jeshi la Niger walimpindua Rais Mohamed Bazoum wa nchi hiyo anayeungwa mkono na Wamagharibi mnamo Julai 26 na kuunda serikali ya mpito.
Mapinduzi hayo ya kijeshi yalifanyika huku kukiwa na wimbi kubwa la chuki dhidi ya Wafaransa, ambao wamekuwa wakituhumiwa kuingilia mambo ya ndani ya Niger.
Niger ina umuhimu mkubwa wa kistratijia ikiwa moja ya wazalishaji wakubwa wa urani ulimwenguni, ambapo wanajeshi wa Ufaransa, Marekani na nchi nyingine za kigeni wametumwa nchini humo kupora utajiri wa nchi hiyo kwa kisingizio cha kupambana na wanamgambo.
Mapema mwezi huu, maelfu ya waandamanaji wanaopinga ubeberu wa Magharibi waliingia barabarani kupinga mipango ya mataifa ya Afrika Magharibi ya kutuma kikosi cha kijeshi katika nchi hiyo kwa kisingizio cha kurejesha utawala wa kikatiba.
Waandamanaji waliizingira kambi ya jeshi la Ufaransa, wakipinga uingiliaji wa kijeshi wa miaka mingi wa nchi hiyo ya Ulaya katika taifa hilo la Afrika Magharibi.
Jeshi la Niger limemtuhumu mkoloni huyo wa zamani kuwa ndiye anayechochea jumuiya ya Afrika Magharibi ECOWAS kuchukua hatua za kutaka kumrejesha madarakani Bazoum ili kutumikia maslahi ya nchi za Magharibi.
Ufaransa ilikuwa mkoloni Afrika Magharibi hadi 1960. Tangu uhuru wa nchi za eneo hilo, nchi hiyo ya Ulaya imedumisha uhusiano wa kibiashara na uwepo wa kijeshi katika eneo hilo.
Kutokana na umuhimu wa nchi hii katika eneo la Sahel Afrika, matukio ya kisiasa nchini Niger yamekabiliwa na radiamali kali kutoka kwa baadhi ya majirani wa Niger pamoja na baadhi ya nchi za nje ya kanda kiasi kwamba ECOWAS (Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi) imetishia kushambulia kijeshi nchi hiyo. Hata hivyo, jumuiya hiyo haijachukua hatua yoyote kuhusiana na suala hili na mazungumzo yanaendelea ili kufikia suluhu ya kidiplomasia. Hata hivyo hadi sasa mazungumzo hayo hayajazaa matunda.
Kwa hakika, nchi za Kiafrika zinajaribu kusuluhisha mzozo wa sasa wa Niger bila uingiliaji wa nchi za kigeni. Wakati huo huo, ECOWAS (Jumuiya ya Kiuchumi ya Afrika Magharibi) inaungwa mkono na nchi za nje kama vile Ufaransa.
Ukweli wa mambo ni kuwa, mgogoro wa sasa wa Niger umesababisha kuibuka misimamo tofauti. Burkina Faso na Mali, ambazo, kama Niger, zinatawaliwa na baraza la kijeshi, zilitangaza kwamba uingiliaji wowote wa kijeshi nchini Niger utakuwa tangazo la vita dhidi yao.
Nchi hizi mbili zikiwa na lengo la kuiunga mkono Niger, zimetuma ndege kadhaa za kijeshi kwenda Niamey, mji mkuu wa Niger, ili kuisaidia serikali ya kijeshi ya Niger. Pia, serikali ya Algeria imepiga marufuku kupita katika anga yake ndege za kivita za Ufaransa zilizokuwa na nia ya kwenda Niger na eneo la Sahel Afrika.
Ukweli wa mambo ni kuwa, raia wengi wa Niger wanaamini kwamba, mapinduzi ya Niger yalikuwa na lengo la kuwafukuza Wafaransa kutoka nchi hii.
Michael Shurkin, mtaalamu mwandamizi mkuu wa Baraza la Atlantiki anasema kuhusiana na hilo: Kwa kutilia maanani historia ya ukoloni barani Afrika, kizazi cha vijana cha Afrika kinaziona nchi za Magharibi kuwa chanzo cha umasikini, ufisadi, fikra finyu za kisiasa barani Afrika na hali ya sasa ya Afrika na kinaiona Ufaransa kuwa msababishaji mkuu wa hali ya sasa.
Kwa upande mwingine, kuendelea kuwa madarakani serikali ya kijeshi nchini Niger hakukubaliki kwa nchi nyingi za eneo na washirika wao wa kigeni; hasa kwa kuzingatia kwamba, hatua hiyo inahatarisha maslahi yao ya kiuchumi na kufanya iwe vigumu kwa wageni kuendelea na uwepo wao wa kijeshi barani Afrika kwa ajili ya kusukuma gurudumu la malengo yao ya kikoloni..
Filihali na katika hatua nyingine, nchi zinazotoa misaada kwa Niger pia zimeamua kusitisha misaada yao kwa nchi hii. ECOWAS pia imesitisha shughuli za kibiashara na benki na Niger na kufungia mali ya nchi hiyo. Joseph Borrell, Mkuu wa Sera za Kigeni na Usalama wa Umoja wa Ulaya, ametangaza kuzuiwa na kufungiwa fedha zilizotengwa na Umoja wa Ulaya kwa Niger.
Ni jambo lisilo na shaka kuwa, utekelezaji wa maamuzi haya utaongeza zaidi mashinikizo ya kiuchumi kwa wananchi na serikali ya Niger, ambayo kimsingi inakabiliwa na matatizo mengi hasa ya kiuchumi.