Jun 20, 2024 11:20 UTC
  • MSF: Sudan inakabiliwa na moja ya migogoro mibaya zaidi duniani

Imeelezwa kuwa, Sudan inakabiliwa na moja ya migogoro mibaya zaidi duniani kuwahi kushuhudiwa katika miongo ya hivi karibuni.

Hayo yameelezwa na Christos Christou. kiongozi wa shirika la kimataifa lisilo la kiserikali la Madaktari Wasio na Mipaka (MSF) ambaye ametahadharisha kuhusu hali mbaya ya kibinadamu inayoikabili nchi hiyo ya Kiafrika.

Ripoti iliyotolewa na MSF inaeleza kuwa, mwaka mmoja baada ya kuanza kwa vita kati ya Jeshi la Serikali la Sudan (SAF) na Vikosi vya Usaidizi wa Haraka (RSF), Sudan inakabiliwa na moja ya migogoro mibaya zaidi katika miongo kadhaa.

Uhai wa mamilioni ya watu kwa sasa unategemea kuhakikisha upatikanaji usiozuiliwa wa kibinadamu, lakini pande pande zinazohasimiana zinaendelea kuzuia kwa makusudi mashirika kufikia walengwa na kutoa misaada. Umoja wa Mataifa na nchi wanachama lazima ziongeze juhudi zao ili kujadili nafasi zaidi na kuongeza mwitikio wa kibinadamu.

Idadi ya wakimbizi Sudan imekuwa ikiongezeka kila siku kutokana na kuendelea kushuhudiwa vita vya wenyewe kwa wenyewe

 

Mapigano ya silaha yalianza huko Sudan Aprili 15 mwaka jana kati ya jeshi la nchi hiyo (SAF)  linaloongozwa na Jenerali Abdel Fattah al Burhan ambaye ni kiongozi wa Sudan na wanamgambo wa Kikosi cha Usaidizi wa Haraka (RSF) ambao kamanda wao ni Hamdan Dagalo.

Hivi karibuni Justin Brady, Mkuu wa ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kuratibu misaada ya kibinadamu (OCHA) nchini Sudan alisema, "leo, Sudan ni mojawapo ya majanga mabaya zaidi ya kibinadamu duniani. Nusu ya wakazi wa Sudan yaani watu milioni 25 wanahitaji msaada wa kibinadamu."