"Afrika CDC" yataka vifaa vya matibabu vitengenezwe ndani ya nchi za Afrika
Jean Kaseya, Mkuŕugenzi Mkuu wa Vituo vya Afŕika vya Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (Afŕika CDC), ameelezea kusikitishwa mno na jinsi nchi za Afrika zilivyo tegemezi kupindukia katika vifaa vya matibabu wakati wa miripuko ya magonjwa.
Akizungumza katika Kongamano la Biashara Huria la Bara la Afrika lililofanyika Kigali, mji mkuu wa Rwanda, Kaseya amesisitizia haja ya bara la Afrika kujizalishia lenyewe chanjo zake, madawa na kujifanyia tafiti za kimatibabu.
"Tumechoshwa na hii hali. Kila wakati unapotokea mripuko wa ugonjwa fulani, tunakuwa na hofu kubwa. Tunalazimika kuhaha na kuomba chanjo, dawa na uchunguzi kutoka kwa wataalamu wa nje ya Afrika. Yaleyale tuliyoyaona wakati wa janga la UVIKO-19 ndiyo hayo hayo tunayoyaona kwenye miripuko ya magonjwa kama Mpox na Marburg. Tumechoka," amesema Kaseya huku akihimiza kuchukuliwa hatua madhubuti za kuweza nchi za Afrika kujitegemea katika chanjo, dawa pamoja na tafiti zake za tiba.

Matamshi yake yamekuja huku kukiwa na mripuko wa ugonjwa wa Marburg (MVD) unaoendelea hivi sasa nchini Rwanda, ambapo kesi 58 zimeshathibitishwa na zimeshasababisha vifo 13.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, pamoja na kwamba Rwanda imechukua hatua madhuburi za kukabiliana na mripuko wa ugonjwa huo, lakini Kaseya amelalamikia vikali ushauri wa hivi karibuni uliotolewa na Marekani ambayo imewataka raia wake wasitembelee Rwanda kwa madai ya kuepuka kuambukizwa virusi vya ugonjwa huo.
Shirika la Afya Duniani linasema kuwa, Marburg (MVD) ni ugonjwa hatari sana wa familia ya Ebola na unasababisha kifo kwa asilimia 88.