Boko Haram waua raia wasiopungua 10 nchini Cameroon
(last modified Thu, 14 Nov 2024 02:45:10 GMT )
Nov 14, 2024 02:45 UTC
  • Boko Haram waua raia wasiopungua 10 nchini Cameroon

Rais wasiopungua 10 wameuawa na wengine kadhaa kujeruhiwa katika shambulizi jipya la genge la kigaidi la Boko Haram nchini Cameroon.

Taarifa hiyo imethibitisha na duru za kieneo za Cameroon ambazo zimesema kuwa, watoto wadogo na wanawake ni miongoni mwa raia 10 waliouliwa kigaidi na genge la Boko Haram wakati genge hilo lilipovamia eneo la kaskazini mwa Cameroon jana Jumatano.

Shambulio hilo la usiku wa kuamkia jana limefanyika katika kijiji cha Ldamang, katika tarafa ya Mayo-Tsanaga kaskazini mwa Cameroon.

Gavana wa Far North Midjiyawa Bakari amethibitisha habari hiyo mbele ya vyombo vya habari na kusema kuwa taarifa zaidi kuhusu shambulio hilo la kigaidi itatolewa baadaye.

Mwezi Septemba mwaka huu pia, magaidi wa Boko Haram walivamia kijiji cha kaskazini mashariki mwa Nigeria wakiwa na pikipiki na kufyatua risasi sokoni na kuteketeza maduka na nyumba sambamba na kuua watu wapatao 127. Taarifa hiyo ilitangazwa na Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Amnesty International na Polisi ya Nigeria.

Shambulio hilo lilitokea Yobe, moja ya majimbo matatu yanayolengwa zaidi na magenge ya kigaidi ambayo yamekuwa yakifanya mauaji ndani ya Nigeria kwa zaidi ya miaka 15 sasa ambapo pia hivi sasa wamepanua wigo wa mashambulizi yao hadi katika nchi jirani za Niger, Cameroon na Chad.