Mapigano makali yaripotiwa jeshi la Sudan likizilenga ngome za mwisho za RFS huko Khartoum
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i124778-mapigano_makali_yaripotiwa_jeshi_la_sudan_likizilenga_ngome_za_mwisho_za_rfs_huko_khartoum
Jeshi la Sudan jana Ijumaa lilikabiliana vikali na hasimu wake yaani Kikosi cha Wanamgambo wa Msaada wa Haraka (RSF) katika ngome za mwisho za kikosi hicho katika mji wa Omdurman huko Khartoum.
(last modified 2025-04-05T07:03:17+00:00 )
Apr 05, 2025 07:03 UTC
  • Mapigano makali yaripotiwa jeshi la Sudan likizilenga ngome za mwisho za RFS huko Khartoum

Jeshi la Sudan jana Ijumaa lilikabiliana vikali na hasimu wake yaani Kikosi cha Wanamgambo wa Msaada wa Haraka (RSF) katika ngome za mwisho za kikosi hicho katika mji wa Omdurman huko Khartoum.

Watu walioshuhudia wameeleza kuwa mapigano makali yalijiri jana kati ya jeshi la Sudan na wanamgambo wa RSF. Mapigano hayo yalianza mapema jana asubuhi katika vitongoji vya magharibi mwa mji wa Omdurman vikiwemo vitongoji vya al Muwaileh, Kandahar and Ombadda. 

Kufuatia mapigano na RSF, wanajeshi wa Sudan walituma kwenye akaunti zao za mitandao ya kijamii picha zikiwaonyesha wakiwa katika kitongoji cha Ombadda katika mji wa Omdurman. 

Mashuhuda wameeleza kuwa: Jeshi la Sudan limekabiliana vikali na wanamgambo wa kikosi cha RSF kusini mwa Omdurman wakati likijaribu kulidhibiti tena eneo hilo. 

Hadi sasa wanamgambo wa RSF hawajatoa taarifa yoyote kuhusu mapigano hayo ya jana.

Hizi ni ngome za mwisho za RSF mjini Khartoum, kwani wiki jana kundi hilo la wanamgambo lilipoteza sehemu kubwa ya eneo lake katika mji mkuu, ikiwa ni pamoja na Ikulu ya Rais.