Serikali ya Sudan yakanusha madai ya kutuma mjumbe huko Israel
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i125028-serikali_ya_sudan_yakanusha_madai_ya_kutuma_mjumbe_huko_israel
Serikali ya Sudan imekanusha kwamba imetuma mjumbe Israel, kufuatia ripoti kwamba mkuu wa Baraza la Mpito la Utawala wa Sudan, Abdel Fattah al-Burhan, alimtuma mjumbe kukutana na maafisa wa serikali ya Tel Aviv.
(last modified 2026-02-25T03:34:48+00:00 )
Apr 11, 2025 04:12 UTC
  • Abdel Fattah al-Burhan
    Abdel Fattah al-Burhan

Serikali ya Sudan imekanusha kwamba imetuma mjumbe Israel, kufuatia ripoti kwamba mkuu wa Baraza la Mpito la Utawala wa Sudan, Abdel Fattah al-Burhan, alimtuma mjumbe kukutana na maafisa wa serikali ya Tel Aviv.

Kanusho hilo la Sudan limetolewa katika taarifa rasmi ya Waziri wa Utamaduni na Habari wa nchi hiyo, Khaled Al-Aiser, ambaye amethibitisha kwamba "kilichoripotiwa na baadhi ya vyombo vya habari kuhusu suala hili ni uongo mtupu."

Taarifa hiyo imesema serikali "inahimiza vyombo vya habari kuwa makini, kutafuta ukweli na kutumia weledi, na kuepuka kuchapisha habari zisizoaminika". 

Awali, magazeti ya Israel yalinukuu ripoti kutoka Sudan, ikiwa ni pamoja na iliyochapishwa na tovuti ya Alrakoba, kwamba wiki iliyopita Burhan alimtuma Luteni Jenerali Sadiq Ismail huko Israel kwa misheni ya siri.

Tovuti hiyo ilidai kuwa mjumbe huyo alikutana na maafisa wa Israel kuandaa mpango "wa kumkurubisha Jenerali Abdel Fattah al-Burhan kwa utawala wa Marekani na kuwasilisha ujumbe kwa Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu kuhusu nia ya Burhan kukamilisha mchakato wa kuanzisha uhusiano na utawala ghasibu wa Israel."

Wakati huo huo, Amer Abbas, mtafiti katika uhusiano wa kimataifa na usalama na masuala ya kijeshi, amesema  kwa kawaida utawala ghasibu wa Israel huchapisha habari kama hizo za mikutano kati ya maafisa wa serikali, hususan maafisa wa Kiarabu na Waislamu na upande wa Israel, kwa lengo la kuzishawishi nchi za Kiarabu kujiunga na mchakato wa kuanzisha uhusiano wa kisiasa na Israel.