Waziri: Iran itajibu ukiukaji wowote wa usitishaji vita
-
Brigedia Jenerali Sayyid Majid Ibn al-Reza
Kaimu Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kuwa, hakiuna shaka yoyote kwamba, Tehran itajibu kwa nguvu zote ukiukaji wowote ule wa usitishaji vita.
Brigedia Jenerali Sayyid Majid Ibn al-Reza, Kaimu Waziri wa Ulinzi wa Iran amesema hayo katika mazungumzo ya simu na Sheikh Saud bin Abdulrahman bin Hassan Al Thani, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nchi anayeshughulikia Masuala ya Ulinzi wa Qatar, ambapo aliishukuru serikali ya Qatar kwa nafasi yake katika mazungumzo yaliyofanikisha usitishaji wa mapigano wa sasa.
Aidha, alisema: "Kwa masikitiko makubwa, upande wa pili tayari umevunja ahadi zake mara kadhaa hata katika kipindi hiki kifupi tangu usitishaji huo wa mapigano uanze."
Amesema,"Vidole vyetu viko kwenye kitufe cha kufyatua risasi, na bila shaka yoyote, endapo kutakuwa na ukiukaji wowote wa masharti ya usitishaji wa mapigano, tutachukua hatua na kutoa jibu linalofaa na la lazima."
Kaimu Wzairi wa Ulinzi wa Iran ameongeza kuwa, "Jamhuri ya Kiislamu sambamba na kuunga mkono kurejea amani na utulivu katika eneo hili, haina imani na Marekani pamoja na utawala wa Kizayuni kutokana na kuvunja ahadi na kuhujumu makubaliano. Endapo kutatokea ukiukaji wowote wa usitishaji wa mapigano, Iran itatoa jibu linalofaa na kuchukua hatua zinazohitajika kulingana na hali husika."
Ameashiria historia ndefu ya Marekani ya kutotimiza ahadi zake kwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kusema:
"Tunao uzoefu wa muda mrefu wa uingiliaji kati na kuvunja ahadi Marekani katika kipindi cha miongo sita hadi saba iliyopita. Masuala yaliyopo kati ya Iran na Marekani yamejengeka juu ya historia ya kutokuaminiana na mwenendo wa mara kwa mara wa uhasama unaofanywa na nchi hiyo."