Gabon wafanya uchaguzi leo; ni wa kwanza baada ya mapinduzi ya kijeshi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i125060-gabon_wafanya_uchaguzi_leo_ni_wa_kwanza_baada_ya_mapinduzi_ya_kijeshi
Wananchi wa Gabon leo Jumamosi wanashiriki kwenye uchaguzi wake wa kwanza wa rais tangu yalipotokea mapinduzi ya kijeshi yaliyomaliza utawala wa miaka 56 ya familia ya Bongo, na kuweka mazingira ya kurejea kwenye utawala wa kiraia katika nchi hiyo ya Afrika ya Kati.
(last modified 2025-04-12T03:05:12+00:00 )
Apr 12, 2025 03:05 UTC
  • Gabon wafanya uchaguzi leo; ni wa kwanza baada ya mapinduzi ya kijeshi

Wananchi wa Gabon leo Jumamosi wanashiriki kwenye uchaguzi wake wa kwanza wa rais tangu yalipotokea mapinduzi ya kijeshi yaliyomaliza utawala wa miaka 56 ya familia ya Bongo, na kuweka mazingira ya kurejea kwenye utawala wa kiraia katika nchi hiyo ya Afrika ya Kati.

Takriban wapiga kura milioni 1.16 wanatarajiwa kushiriki kwenye uchaguzi wa leo utakaoendelea hadi saa 11 jioni. Hii inajumuisha takriban wapiga kura 860,000 waliojiandikisha wakati wa kura ya maoni ya katiba mpya mwaka 2024, pamoja na wapiga kura wapya 300,000 - wengi wao wakiwa ni vijana ambao wanapiga kura kwa mara ya kwanza.

Mwezi Novemba mwaka jana, nchi hiyo iliitisha kura ya maoni na kuidhinisha katiba mpya, inayotazamwa na wengi kama hatua muhimu katika kuelekea uchaguzi wa kidemokrasia. Kura hiyo ilifanyika baada ya kupita zaidi ya mwaka mmoja wa kutokea mapinduzi ya mwezi Agosti 2023 ambayo yalimuondoa madarakani Rais Ali Bongo na kumweka madarakani Jenerali Brice Oligui Nguema.

Gabon, Jenerali Brice Oligui Nguema

 

Tofauti na kura za huko nyuma zilizotawaliwa na machafuko, kupingwa, maandamano, kukatwa mawasiliano na amri ya kutotoka nje - uchaguzi wa leo unatarajiwa kufanyika kwa utulivu na amani. Kipindi cha mpito cha baada ya mapinduzi ya kijeshi nchini Gabon kimechukua miezi 18. 

Kwa mara ya kwanza baada ya zaidi ya miongo mitano, jina la Bongo litakosekana kwenye orodha ya wagombea. Baadhi ya wagombea lakini wanasema kuwa bado kivuli cha familia ya Bongo kimetanda kwa sababu ya mtazamo wa mfumo wa kisiasa wa kiukoo.

Rais wa serikali ya mpito Jenerali Brice Oligui Nguema ameruhusiwa na Katiba mpya kugombea. Mpinzani wake mkuu ni Alain-Claude Bilie-By-Nze, waziri mkuu wa zamani katika serikali ya Ali Bongo.