Uhusiano na mkoloni Ufaransa wazidi kuharibika, Algeria yamwita balozi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i125142-uhusiano_na_mkoloni_ufaransa_wazidi_kuharibika_algeria_yamwita_balozi
Wizara ya Mambo ya Nje ya Algeria imemwita balozi wa Ufaransa mjini Algiers, Stephane Romatet ili kujieleza ikiwa ni kuonesha malalamikio makali ya Algiers kuhusu kuzuiliwa balozi mdogo wa Algeria nchini Ufaransa.
(last modified 2026-04-19T09:26:01+00:00 )
Apr 13, 2025 22:52 UTC
  • Uhusiano na mkoloni Ufaransa wazidi kuharibika, Algeria yamwita balozi

Wizara ya Mambo ya Nje ya Algeria imemwita balozi wa Ufaransa mjini Algiers, Stephane Romatet ili kujieleza ikiwa ni kuonesha malalamikio makali ya Algiers kuhusu kuzuiliwa balozi mdogo wa Algeria nchini Ufaransa.

Jumamosi serikali ya Ufaransa ilimweka kizuizini kwa muda balozi wa Algeria kwa madai ya kuhusishwa na tukio la mwaka 2024 la kutekwa nyara Amir Boukhras, mwanaharakati aliyekuwa anasakwa wa Algeria aliyekuwa anaishi Paris na ambaye ni maarufu kwenye mitandao ya kijamii kwa jina la "AmirDZ."

Katika taarifa yake ya kulalamikia hatua hiyo ya Paris, Algiers imesema madai yaliyotolewa na Ufaransa ya kuhalalamisha "ufedhuli" wake huo hayana msingi wowote ikisisitiza kwamba balozi huyo ana kinga ya kidiplomasia na kwamba alikamatwa Jumamosi hadharani bila ya kutolewa taarifa yoyote ya kidiplomasia na huo ni ukiukaji mkubwa sana usio na kifani na usio na msingi wa sheria za kimataifa zinazowalinda wanadiplomasia.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Algeria imeongeza kuwa ushahidi pekee uliotolewa na serikali ya Ufaransa, ni kupatikana simu ya mkononi ya afisa huyo karibu na makazi ya Boukhras.

Algeria imetaka kuachiliwa huru mara moja balozi wake huyo, ikionya kwamba vitendo kama hivyo vya serikali ya Paris vinadhooofisha juhudi za hivi karibuni za kurejesha uhusiano wa pande mbili, ikiwa ni pamoja na makubaliano yaliyofikiwa wakati wa mazungumzo ya simu kati ya viongozi wakuu wa nchi hizo mbili.

Inaonekana Ufaransa hadi hivi sasa ina kiburi kilekile cha enzi za ukoloni cha mkoloni na mkoloniwa, lakini nchi za Afrika kwa miaka kadhaa sasa zimeionesha Ufaransa kwamba hali imebadilika na hizi si zama tena za mkoloni huyo wa Ulaya kufanya chochote tu inachotaka barani Afrika.