Ripoti: Wanawake walidhulumiwa wakati na baada ya vita vya Tigray
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i129116
Unyanyasaji wa kingono na mateso kwa kina mama na wasichana kupewa mimba za kulazimishwa yalifanyika wakati na baada ya vita katika eneo la Tigray nchini Ethiopia.
(last modified 2025-08-04T05:09:25+00:00 )
Aug 04, 2025 02:34 UTC
  • Ripoti: Wanawake walidhulumiwa wakati na baada ya vita vya Tigray

Unyanyasaji wa kingono na mateso kwa kina mama na wasichana kupewa mimba za kulazimishwa yalifanyika wakati na baada ya vita katika eneo la Tigray nchini Ethiopia.

Mashirika mawili yasiyo ya kiserikali ya kutetea haki za binadamu yameeleza katika ripoti yao inayojumuisha "uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu."

Ripoti hiyo imesema eneo la kaskazini mwa Ethiopia lilikabiliwa na vita vya kikatili vya wenyewe kwa wenyewe kuanzia mwaka 2020 hadi 2022, ambapo vikosi vya serikali ya Ethiopia, vilivyoungwa mkono na jeshi la Eritrea na wanamgambo wa ndani, vilihusika dhidi ya chama cha siasa cha eneo hilo, cha Tigray People's Liberation Front (TPLF).

Ripoti zinasema, watu wapatao 600,000 walikufa wakati wa vita hivyo, na pande zote zililaumiwa kwa kufanya ukatili.

Ripoti hiyo ya kurasa 88 iliyoandaliwa na kundi la Madaktari wa Haki za Binadamu (PHR) na Shirika la Haki na Uwajibikaji katika Pembe ya Afrika (OJAH) inajumuisha mahojiano na wafanyakazi wapatao 500 wa huduma za afya na maafisa wa mashirika ya kutetea haki za binadamu yamesaidia kufichua matendo ya unyanyasaji yaliyofanywa kwa makusudi ambayo yanahusiana na unyanyasaji wa kingono na kuwapa wanawake mimba zisizotakiwa.

Mashirika ya kutetea haki ya PHR na OJAH yamesema kwenye ripoti yao kwamba:

"Vitendo hivyo vinajumuisha uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu kutokana na unyanyasaji wa kingono, mimba za kulazimishwa, utumwa wa kingono na mateso kwa kuzingatia misingi ya kikabila, jinsia, umri na misimamo ya kisiasa."