UN yataka nchi za Afrika zishirikiane kijeshi ili kudumisha amani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i130004-un_yataka_nchi_za_afrika_zishirikiane_kijeshi_ili_kudumisha_amani
Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Amina J. Mohammed, amewataka viongozi wa kijeshi wa Afrika kushirikiana kwa karibu zaidi ili kukabiliana na ongezeko la vitisho vya usalama, ugaidi na athari za mabadiliko ya tabianchi katika bara hilo.
(last modified 2025-08-26T05:58:28+00:00 )
Aug 26, 2025 05:58 UTC
  • UN yataka nchi za Afrika zishirikiane kijeshi ili kudumisha amani

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Amina J. Mohammed, amewataka viongozi wa kijeshi wa Afrika kushirikiana kwa karibu zaidi ili kukabiliana na ongezeko la vitisho vya usalama, ugaidi na athari za mabadiliko ya tabianchi katika bara hilo.

Akizungumza katika Mkutano wa kwanza wa wakuu wa majeshi ya ulinzi barani Afrika jijini Abuja nchini Nigeria Jumatatu amesema mkutano huo unaashiria “kuzaliwa kwa enzi mpya ya ushirikiano wa kiusalama barani Afrika.”

Bi. Mohammed ameongeza kuwa “Kila mmoja kati ya watu bilioni 1.4 wa Afrika anastahili kuishi kwa usalama na heshima. Hii inamaanisha kulinda raia, kuheshimu mipaka, na kusimamia kanuni za sheria za kimataifa na Mkataba wa Umoja wa Mataifa. Zaidi ya yote, inahitaji mshikamano dhidi ya vitisho vyetu vya pamoja.”

Bi. Mohammed ameonya kuwa Afrika bado ndiyo kitovu cha vifo vinavyosababishwa na ugaidi duniani, huku makundi tanzu ya Al-Qaida na Daesh (ISIS) yakipanua wigo wa ushawishi wao barani humo.

Pia amebainisha ongezeko la asilimia 250 ya mashambulizi katika nchi za pwani za Afrika Magharibi ndani ya miaka miwili pekee, na kufungwa kwa zaidi ya shule 14,000 katika Ukanda wa Sahel ya Kati kutokana na mapigano.

Ameonya kuwa “Wakati vijana wanaposhindwa kuona njia ya elimu au haki, propaganda za kigaidi hupata wasikilizaji”. Hivyo amesisitiza kuwa “Tuko hatarini kupoteza kizazi kizima tusipochukua hatua.”

Naibu Katibu Mkuu huyo amesisitiza kuwa teknolojia mpya kuanzia ndege zisizo na rubani au drooni hadi akili mnemba zinabadilisha sura ya vita. Amesema ingawa Akili Mnemba inatoa suluhisho kama vile kugundua mabomu yaliyotegwa ardhini au kutabiri wimbi la wakimbizi, pia inaleta hatari za mashambulizi ya kimtandao, matumizi mabaya ya ufuatiliaji, na ukiukaji wa haki za binadamu. 

Afisa huyo mwandamizi wa Umoja wa Mataifa ambaye ni raia wa Nigeria halikadhalika ameonya kuwa: “Mtandao wa intaneti sasa ni uwanja wa vita."

Aidha amesema: “Mashambulizi ya kimtandao yanayowezeshwa na Akili Mnemba yanaweza kulemaza miundombinu muhimu na kusimamisha huduma za msingi. Hatuwezi kubaki watazamaji. Afrika lazima ichukue usukani na kuamua jinsi teknolojia hizi zitakavyotumika.”

Aidha, ameongeza kuwa mabadiliko ya tabianchi tayari ni “tishio la moja kwa moja kwa amani,” yakisababisha mamilioni ya watu kukimbia makazi yao katika Bonde la Ziwa Chad, kuongeza upungufu wa chakula na kuchochea migogoro ya kugombea rasilimali.

Akihitimisha hotuba yake, Mohammed amewataka viongozi wa Afrika kuwatambua wanawake na vijana kama wadau muhimu wa kujenga amani, na si waathirika pekee wa migogoro.

Mkutano huo uliowaleta pamoja wakuu wa majeshi ya ulinzi kwa ajili ya kushughulikia changamoto za kiusalama barani Afrika na kuimarisha ushirikiano utamalizika Agosti 27.