Maafisa wa jeshi la DR Congo wasailiwa huku mapigano yakishadidi eneo la mashariki
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i130006-maafisa_wa_jeshi_la_dr_congo_wasailiwa_huku_mapigano_yakishadidi_eneo_la_mashariki
Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo lilitangaza Jumatatu kwamba maafisa 41 wa ngazi za juu jeshini wamesailiwa kama sehemu ya uchunguzi kuhusu kushindwa kwa vikosi vya serikali wakati wa mapigano dhidi ya waasi wa M23 katika eneo la mashariki la nchi hiyo lenye machafuko.
(last modified 2025-08-26T09:11:38+00:00 )
Aug 26, 2025 06:00 UTC
  • Maafisa wa jeshi la DR Congo wasailiwa huku mapigano yakishadidi eneo la mashariki

Jeshi la Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo lilitangaza Jumatatu kwamba maafisa 41 wa ngazi za juu jeshini wamesailiwa kama sehemu ya uchunguzi kuhusu kushindwa kwa vikosi vya serikali wakati wa mapigano dhidi ya waasi wa M23 katika eneo la mashariki la nchi hiyo lenye machafuko.

Wale walioitwa kusailiwa katika Ofisi ya Ukaguzi wa Majeshi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ni pamoja na majenerali 35 na makanali 6, amesema msemaji wa jeshi, Meja Jenerali Sylvain Ekenge, akizungumza na waandishi wa habari.

Amesema mchakato huu unahusu maafisa wote waliokuwa na nyadhifa za uongozi tangu kuchukuliwa kwa mji wa mpakani wa Bunagana na waasi wa M23 mnamo Juni 2022.

Kwa mujibu wa Ekenge, uchunguzi huo unalenga kubaini majukumu ya kila afisa katika kushindwa kwa jeshi kwenye vita vya uwanja wa mapigano.

Hayo yanajiri huku serikali ya DRC na waasi wa M23 wakilaumiana kwa kukiuka makubaliano ya kusitisha mapigano, wakati mazungumzo yanaendelea nchini Qatar kwa lengo la kumaliza mzozo huo.

Mwaka jana, mahakama ya kijeshi mashariki mwa Congo iliwahukumu kifo wanajeshi 25 kwa "kutoroka badala ya kukabiliana na adui" wakati wa mapigano na waasi wa M23.

Tangu 2021, waasi wa M23 wanaohusishwa na uasi mashariki mwa Congo, wameteka maeneo makubwa, miji muhimu ya Goma na Bukavu, ambayo ilitekwa mapema mwaka huu.

Umoja wa Mataifa, na serikali ya DRC wanaituhumu Rwanda kwa kuunga mkono M23, jambo ambalo serikali ya Kigali inalikana. Eneo hilo la mashariki mwa DRC lina madini ambayo ni muhimu sana kwa teknolojia za kisasa ina inaaminika kuwa madola ya Magharibi yanachochea vita ili kuendelea kupora utajiri huo wa madini.