Mwanaharakati mtetezi wa haki Kenya atangaza kujitosa kwenye kinyang'anyiro cha urais 2027
Mwanaharakati maarufu wa kutetea haki nchini Kenya Boniface Mwangi ametangaza kwamba atawania urais katika uchaguzi mkuu wa 2027.
Akibainisha maono ya sera zake katika Jumba la Ufungamano jijini Nairobi hapo jana, Mwangi ameahidi kukabiliana na tabaka la kisiasa lililokita mizizi na kuifkisha sauti ya mwanaharakati ndani ya Ikulu ya nchi hiyo.
Mwanaharakati huyo ameahidi kuzipa kipaumbele huduma bora za afya, elimu bila ya malipo, uwajibikaji na haki kwa waathiriwa wa ukatili wa serikali na upatikanaji wa uhakika wa mahitaji muhimu kama vile maji safi.
"Leo, Siku ya Katiba, natangaza nia yangu ya kugombea urais 2027. Mustakabali wa nchi yetu uko mikononi mwetu na si mikononi mwa mtu mwingine," alieleza Mwangi.
Siku ya Katiba, ya kuadhimisha Katiba ya Kenya ya mwaka 2010, ilitangazwa hivi majuzi na Rais William Ruto kuwa ni ya maadhimisho ya kitaifa, lakini si sikukuu rasmi ya umma, itakayoadhimishwa kwa shughuli za kiraia katika taasisi zote za serikali, maskulini na katika taasisi za kidiplomasia za nchi hiyo nje ya nchi, ikithibitisha tena kujitolea kwa Wakenya kushikamana na utawala wa sheria.
Mwangi, mwenye umri wa miaka 42, alipata umaarufu baada ya kuakisi ghasia za baada ya uchaguzi wa 2007 - 2008 akiwa mwanahabari mpigapicha. Kazi hiyo ilimfanya atambuliwe kimataifa lakini pia ilimtumbukiza kwenye mzozo na mikwaruzano na watu mashuhuri wa kisiasa.
Katika miaka iliyofuata, aliongoza kampeni za kupinga ufisadi, akaandaa maandamano yaliyoongozwa na vijana na akawa mkosoaji mkubwa wa serikali zilizofuata, akisema siasa za Kenya zimetawaliwa na nasaba za watu na mitandao ya wafadhili.
Tamko hilo la Mwangi la kuwania urais mwaka ujao limetolewa wakati maandamano ya mitaani, ambayo mara nyingi huongozwa na wanaharakati wa Gen Z, yametibua mfumo tawala wa kisiasa wa Kenya. Wadadisi wa mambo wanahisi kugombea kwake kunaweza kuchochea upigaji kura utakaoakisi hisia za maandamano hayo ya upinzani au kudhihirisha mipaka ya ushawishi wa siasa za uanaharakati katika uchaguzi wa nchi hiyo.
Wakenya watapiga kura 2027 katika uchaguzi unaotarajiwa kuwa na upinzani mkali, ambapo Rais Ruto atawania kuchaguliwa tena kwa muhula wa pili.../