Afrika Kusini: Mauaji ya Wapalestina yameongezeka sana, Israel inapaswa kusitisha vita
Afrika Kusini imesema mauaji ya Wapalestina yanazidi kuongezeka na hivyo imeutaka utawala wa Israel uafiki mkataba wa kusitisha mapigano uliojadiliwa na wadau wote muhimu.
Ronald Lamola, Waziri wa Mambo ya Nje wa Afrika Kusini ametoa kauli hiyo katika mkutano wa waandishi wa habari katika mji mkuu Pretoria na kuongeza kwamba: "Afrika Kusini inarudia wito wake wa kusitishwa mapigano mara moja huko Gaza. Mauaji ya Wapalestina yanaendelea kuongezeka kwa kiwango kikubwa na tunasisitiza kuwa kusitishwa kwa mapigano ni muhimu ili kudhibiti janga la kibinadamu."
Lamola ameongeza kwamba: "Ripoti ya pamoja ya mashirika manne ya Umoja wa Mataifa imethibitisha hofu zetu kwamba kushindwa kutekelezwa hatua za kusitisha mapigano ambazo zilitangazwa kufuatia kesi ya Afrika Kusini katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) kumeibua baa la njaa ambalo limesababishwa na binadamu."
Amesema kwamba njia zinazohitajika kuendeleza maisha huko Gaza zinaharibiwa, jambo ambalo ni ushahidi zaidi wa dhamira ya kuteketeza mauaji ya kimbari.
Afrika Kusini ilifungua kesi dhidi ya Israel mwishoni mwa 2023 katika ICJ huko The Hague, kwa msingi kwamba utawala wa Israel haujatekeleza ahadi zake chini ya Mkataba wa 1948 wa Kuzuia Mauaji ya Kimbari.
Israel imemuua karibu Wapalestina 64,000 huko Gaza tangu ianzishe vita vya mauaji ya kimbari katika eneo hilo Oktoba 2023. Vizuwizi kamili vya Israel dhidi ya kambi ya Wapalestina, vilivyowekwa tangu mapema Machi, vimeleta hali mbaya kwa wakazi milioni 2.4 wa eneo hilo, na kusababisha njaa, magonjwa yanayoshadidi na kuporomoka kwa huduma muhimu.
Mwaka jana, Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC) ilitoa hati za kukamatwa Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Waziri wa zamani wa vita Yoav Gallant kwa jinai za kivita na uhalifu dhidi ya binadamu huko Gaza.