Rwanda yakiri kuwa imepokea wahamiaji saba waliotimuliwa Marekani
Rwanda imekiri kuwa imepokea wahamiaji saba waliotimuliwa nchini Marekani mapema mwezi huu.
Msemaji wa serikali Yolande Makolo amethibitisha hilo kupitia taarifa aliyotoa jana Alkhamisi, zikiwa zimepita wiki chache tangu nchi hizo mbili zilipofikia makubaliano ya kuhamisha hadi watu 250.
“Kundi la kwanza la wahamiaji saba waliokaguliwa liliwasili Rwanda katikati ya mwezi Agosti. Watu watatu kati yao wameonesha nia ya kurejea katika nchi zao za asili, huku wanne wameamua kubaki na kujenga maisha yao nchini Rwanda. Bila kujali mahitaji yao binafsi, watu hawa wote watapatiwa msaada unaofaa na ulinzi kutoka kwa serikali ya Rwanda”, amesema Makolo.
Mapema mwezi huu, msemaji huyo wa serikali ya Kigali alitangaza kuwa, chini ya makubaliano hayo iliyofikia Rwanda na Marekani, wahamiaji watakaotimuliwa na kupelekwa nchini humo watapatiwa mafunzo ya kazi, huduma za afya, na makazi.
Katika miaka ya hivi karibuni, Rwanda imejitangaza kama nchi inayowakaribisha wahamiaji wanaotakiwa kuondolewa na mataifa ya Magharibi, licha ya wasiwasi wa mashirika ya haki za binadamu kuwa Kigali hailipi umuhimu wa kutosha suala la kuheshimu haki za msingi za binadamu…/