China, Iran na Russia zathibitisha; Muda wa Azimio Nambari 2231 umemalizika
Iran, China na Russia zimemwandikia barua ya pamoja Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, kuthibitisha kumalizika muda wa Azimio Nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa (UNSC) kuhusu mpango wa amani wa nishati ya nyuklia wa Jamhuri ya Kiislamu.
Barua hiyo iliyoandikwa na wajumbe wa kidiplomasia wa waitifaki hao wa Iran kwa shirika hilo kubwa la dunia, imetumwa kwa Antonio Guterres juzi Ijumaa.
Washirika hao walisema "wanathibitisha kwamba kwa mujibu wa kipengee cha 8 cha utekelezaji wa Azimio 2231, masharti yake yote yatakomeshwa baada ya tarehe 18 Oktoba 2025."
Kwa hivyo, tarehe hiyo "inaashiria mwisho wa Baraza la Usalama kuzingatia suala la nyuklia la Iran," wanadiplimasia wa Iran, China na Russia wameeleza.
Azimio hilo liliidhinisha Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA), makubaliano ya kihistoria ya nyuklia ya mwaka 2015 kati ya Iran na mataifa mengine. Baada ya kuidhinishwa, liliagiza kusimamishwa vikwazo vinavyohusiana na nyuklia dhidi ya Jamhuri ya Kiislamu.
Abbas Araghchi, Waziri wa Mashauri ya Kigeni wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, amesema katika barua rasmi hiyo kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres na Mwenyekiti wa Kiduru wa Baraza la Usalama Vassily Nebenzia kwamba, vipengee vilivyo wazi vya azimio nambari 2231 na kusisitiza kuwa, suala la miradi ya nyuklia ya Iran linapaswa kuondolewa katika ajenda za Baraza la Usalama baada ya miaka kumi na kwamba kuanzia sasa hakuna msingi wowote wa kisheria wa kuwekea vikwazo mpango wa nyuklia wa Iran.
Aidha Mapema jana, Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Iran ilitoa tamko kuhusiana na kumalizika muda wa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kusema: Vikwazo vilivyowekwa dhidi ya mpango wa nyuklia wa Iran vinamalizika Jumamosi Oktoba 18, 2025.