Afrika CDC: Mpox bado ni dharura ya kiafya barani Afrika
-
Mgonjwa wa Mpox
Ugonjwa wa Mpox ambao umeenea katika nchi za Kiafrika na kuua mamia ya watu, bado ni dharura ya kiafya katika bara hilo. Taarifa hii imetolewa na Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Barani Afrika (Africa CDC).
Afrika CDC imeeleza haya baada ya kundi la mashauriano kugundua ongezeko jipya la wagonjwa wa Mpox katika nchi nyingi za bara la Afrika.
Afrika CDC imesema katika taarifa yake kuwa Kundi la Ushauri wa Dharura ambalo humshauri Mkurugenzi Mkuu wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa Afrika kuhusu ugonjwa wa Mpox, limekishauri Kitengo cha Dharura ya Afya barani Afrika kukusanya rasilimali na kuziandaa nchi kuchukua hatua za tahadhari mkabala wa maambukizo ya Mpox.
Mapitio yaliyofanywa na Kundi la Ushauri wa Dharura yanaonyesha kuwa hali ya mambo inaashiria kuwa kulikuwa na ongezeko la maambukizi ya ugonjwa wa Mpox katika nchi kama Ghana, Liberia, Kenya, Zambia na Tanzania
Aidha kujitokeza upya kwa virusi vya ugonjwa huo kuripotiwa huko Malawi, Ethiopia, Senegal, Togo, Gambia na Msumbiji.
Kundi la Ushauri wa Dharura ambalo lilihitimisha katika mkutano wake tarehe Pili mwezi huu wa kutazama upya hali ya mlipuko na kutathmini iwapo hali ya dharura inapaswa kuondolewa au la, kwamba ni muhimu kuendelea kuwekwa wazi suala hilo.
Vilevile limetaka kuchunguzwa zaidi vifo vlivyosababishwa na ugonjwa wa Mpox hususan miongoni mwa watoto na kupanuliwa upatikanaji wa huduma ya chanjo kwa watoto walio na umri wa miaka chini ya 12 katika nchi zilizo katika hatari kubwa.
Taarifa iliyotolewa jana wa Afrika CDC ilieleza kuwa kesi 185,994 za Mpox zimeripotiwa katika nchi 20 barani Afrika tangu kuanza mwaka uliopita.