UN yasikitishwa na shambulio la droni lililoua zaidi ya raia 30 Sudan
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres, amesikitishwa sana na shambulio la droni yaani ndege isiyo na rubani lililoua raia wasiopungua 30 katika Jimbo la Darfur Kusini, huko Sudan.
Shambulio hilo limeripotiwa kutokea katika eneo lililoko takriban kilomita 150 kusini-magharibi mwa makao makuu ya jimbo hilo yaani mji wa Nyala.
Farhan Haq, Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amethibitisha habari hiyo na kusema kuwa, Antonio Guterres amehimiza pande zote kusimamisha vita na kuruhusu kufikiwa maeneo yaliyoathiriwa vibaya na mapigano huko Sudan. Amesema: Shambulio la hivi sasa limekuja huku mapigano yakiongezeka katika maeneo ya Darfur na Kordofan, hasa mashambulizi ya droni yanayoongezeka kwa kasi kwenye maeneo hayo.
Aidha amesema: "Katibu mkuu (wa UN) analaani mashambulizi yote dhidi ya raia na miundombinu ya raia, na anazitaka pande zote zitekeleze wajibu wao chini ya sheria za kimataifa, ikiwa ni pamoja na sheria za kimataifa za masuala ya kibinadamu na sheria za kimataifa za haki za binadamu, katika maeneo yote ya migogoro nchini Sudan."
Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ameongeza kuwa, katibu mkuu anarudia mwito wake kwa mataifa yote yenye ushawishi kwa pande mbili zinazopigana huko Sudan, kuzilazimisha zisimamishe vita mara moja na zizuie kumiminwa silaha huko Sudan.
Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF na Jeshi la Sudan SAF vilianza kupigana tarehe 15 Aprili 2023 kutokana na uchu wa madaraka. Mgogoro wa Sudan umeshapelekea makumi ya maelfu ya watu kuuawa na mamilioni ya wengine kuhama makazi yao. Sudan hivi sasa ina moja ya migogoro mibaya zaidi ya kibinadamu duniani.