ISIL yatangaza kuhusika na shambulio baya nchini Syria
Kundi la kigaidi la ISIL (Daesh) limedai kuhusika na shambulio baya lililolenga vikosi vitiifu kwa Abu Mohammad al-Jolani nje kidogo ya Idlib, kaskazini magharibi mwa Syria.
Kwa mujibu wa chombo cha habari kinachohusiana na shirika la kigaidi la ISIL, wanamgambo wa kundi hilo wamevishambulia vikosi vinavyohusiana na Jolani katika barabara ya Maarrat al-Numan nje kidogo ya mkoa wa Idlib nchini Syria.
Ripoti hiyo imesema shambulio hilo limesababisha mauaji ya wanachama wanne wa vikosi vilivyolengwa huku wengine kadhaa wakijeruhiwa. Imedai kwamba washambuliaji walifanikiwa kuondoka salama na kurudi katika nafasi zao kufuatia operesheni hiyo.
Mapema Jumapili, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Syria ilithibitisha kwamba angalau wanajeshi wanne wanaohusishwa na utawala wa Jolani waliuawa katika shambulio la silaha katika mji wa Maarrat al-Numan, ulioko kusini mwa Idlib.
Wizara hiyo imesema vikosi vya usalama vimeanzisha shughuli za utafutaji na upekuzi katika eneo hilo ili kuwatambua na kuwakamata waliohusika na shambulio hilo.
Tukio hilo linakuja huku kukiwa na makabiliano ya silaha na mvutano wa ndani nchini Syria, ambao umeendelea tangu kupinduliwa kwa serikali ya Bashar al-Assad, licha ya operesheni za usalama zinazoendelea katika maeneo kadhaa.