Jul 17, 2024 13:17 UTC
  • Daesh: Tumehusika na shambulio la siku ya Ashura lililoua 6 Oman

Kundi la kigaidi la Daesh (ISIS) limekiri kuhusika na shambulizi la kigaidi lililolenga Waislamu wa madhehebu ya Shia waliokuwa wamekusanyika katika msikiti mmoja nchini Oman, kwa ajili ya maombolezo ya Ashura ya kukumbuka siku ya kuuliwa shahidi mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW), Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (a.s).

Katika taarifa ya jana usiku, Daesh imetangaza kuwa, wapiganaji wake watatu waliwafyatulia risasi waumini waliokuwa msikitini kwa ajili ya marasimu ya Ashura nje ya Msikiti wa Imam Ali AS katika wilaya ya Wadi Kabir, nje kidogo ya mji mkuu wa Oman, Muscat.

Kundi hilo la kigaidi limesambaza kwenye mtandao wa kijamii wa Telegram video inayoonyesha Waislamu wakikimbia huku na kule wakati wa shambulio hilo la usiku wa kuamkia jana; ambapo magaidi hao walikabiliana kwa risasi na askari polisi wa Oman hadi asubuhi.

Watu tisa, wakiwemo raia wanne wa Pakistan, mmoja wa India na afisa wa polisi ni miongoni mwa watu waliouawa katika shambulio hilo la kigaidi lililolenga waombolezaji wa Ashura ya Imam Hussein AS nchini Oman. Jeshi la Polisi la Oman limesema watu wasiopungua 28 walijeruhiwa kwenye shambulio hilo.

Magaidi wa Daesh

Jumanne ya jana ilikuwa siku ya Ashura, mwezi kumi Mfunguo Nne Muharram ambayo ni siku ya majonzi makubwa kwa Ahlul Bayt wa Mtume SAW na kwa kila mpenda haki duniani. Mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW), Imam Hussein AS na masahaba zake 72, waliuawa shahidi na kidhulma na jeshi la mtawala dhalimu Yazid mwana wa Muawiya katika jangwa la Karbala, kusini mwa Iraq mwaka 680 Milaadia, baada ya kupigana kwa ujasiri na ushujaa mkubwa mno.

Mapambanao ya Karbala hadi leo yamekuwa ni nembo ya ushindi wa damu dhidi ya upanga, na ni nembo ya kila anayepambana na dhulma ulimwenguni. 

Tags