Jumapili, Septemba 28, 2025
Leo ni Jumapili tarehe 5 Mfunguo Saba Rabiu Thani 1447 Hiijria mwafaka na tarehe 28 Septemba 2025 Miladia.
Katika siku kama ya leo miaka 180 iliyopita mwafaka na tarahe 5 Mfunguo Saba Rabiu Thani mwaka 1267 Hijiria, gazeti la kwanza la lugha ya Kifarsi lililoitwa 'Waqai'e Itifaqiyeh' lilianza kuchapishwa mjini Tehran. Gazeti hilo lilianza kuchapishwa wakati wa kutimia mwaka wa tatu wa ufalme wa Nasiruddin Shah Kajjar, kwa amri ya Kansela Mirza Taqi Khan Amir Kabir. Gazeti hilo lilikuwa likiandika habari za utawala wa wakati huo wa Iran, dunia na makala za kisayansi zilizokuwa zikitafsiriwa kutoka kwenye magazeti ya Ulaya. Gazeti la 'Waqai'e Itifaqiyeh' lilichapisha hadi toleo nambari 472 na baada ya hapo liliendelea kuchapishwa kwa majina tofauti.

Siku kama ya leo miaka 130 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Louis Pasteur, tabibu na mwanakemia wa Kifaransa. Akiwa shuleni alisoma kwa bidii na jitihada kubwa. Baada ya kumaliza masomo yake alifanikiwa kupata shahada ya uzamivu katika kemia na kuanza kufundisha katika Chuo Kikuu cha Strasbourg huku akijihusisha uhakiki na utafiti kuhusiana na masuala mbalimbali ya kielimu.

Siku kama ya leo miaka 55 iliyopita, alifariki dunia rais wa zamani wa Misri, Gamal Abdel Nasser. Abdel Nasser alizaliwa mwaka 1916. Alishiriki katika vita vya kwanza vya Waarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel hapo mwaka 1948 na kufanya mapinduzi ya kijeshi kwa kushirikiana na Jenerali Najib, dhidi ya Mfalme Faruq 1952 na kuung'oa utawala wa kisultani nchini humo. Miaka miwili baadaye Gamal Abdel Nasser alimuondoa madarakani mshirika wake Jenerali Najib na kuchukua jukumu la kuiongoza Misri sanjari na kufanya juhudi za marekebisho, kupambana na ukoloni na utawala ghasibu wa Israel. Mwaka 1956 aliutaifisha mfereji wa Suez na kuufanya kuwa mali ya Misri, hatua iliyozifanya nchi za Ufaransa, Uingereza na utawala wa Kizayuni kuishambulia Misri. Hatua ya viongozi wa Misri ya kujibu hujuma hiyo, iliongeza umaarufu wa Abdel Nasser nchini Misri na ulimwenguni kwa ujumla.

Miaka 105 iliyopita siku hii yaani Septemba 28, 1920, nchi ya Oman ilitangaza uhuru wake kutoka kwa mkoloni wa Ulaya, Uingereza na siku hii iliitwa Siku ya Uhuru kwa taifa la Oman. Nchi ya Oman iko kusini mwa Ghuba ya Uajemi na Bahari ya Oman, na iko jirani na nchi za Saudi Arabia, Muungano wa Falme za Kiarabu na Yemen. Nchi hiyo ilitekwa na majeshi ya kikoloni ya Ureno mwaka 1508 na baada ya miaka mia moja na khamsini, yaani mwaka wa 1659, ikawa chini ya udhibiti wa Dola ya Uthmania (Ottoman Empire). Baada ya hapo, ardhi ya Oman iliingia mikononi mwa watawala kadhaa wa ndani ya Oman na Ufalme wa Afsharid wa Iran hadi ilipoingia kwenye himaya ya Uingereza mwishoni mwa karne ya 18 na ilichukuliwa rasmi na wakoloni wa Uingereza mwaka 1820. Hatimaye, karne moja baadaye, yaani tarehe 28 Septemba, 1920, mkataba unaojulikana kwa jina la "Mkataba wa Seeb" ulitiwa saini ya viongozi wa nchi mbili na uhuru wa Oman ukatambuliwa rasmi baada ya kupita karne nzima, yaani miaka mia moja.

Katika siku kama ya leo miaka 29 iliyopita, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lilitoa azimio likiutaka utawala wa Kizayuni wa Israel kukomesha operesheni ya kuchimba mashimo chini ya Msikiti wa al Aqsa huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Azimio hilo lililaani uchimbaji huo wa mashimo kinyume cha sheria chini ya eneo hilo takatifu. Hata hivyo upinzani wa Marekani ulipelekea kuondolewa kipengee hicho katika azimio hilo. Uchimbaji huo wa mashimo chini ya Msikiti wa al Aqsa na utawala huo ghasibu, ulizusha machafuko ya umwagaji damu mkubwa hapo tarehe 23 Septemba 1996 kati ya askari wa Israel na Wapalestina ambapo askari hao waliua na kujeruhi mamia ya Wapalestina.

Siku kama ya leo miaka 24 iliyopita Intifadha ya wananchi wa Palestina kwa mara nyingine tena ilipamba moto. Hatua ya Ariel Sharon kiongozi wa chama chenye misimamo mikali cha Likud na mhusika mkuu wa mauaji ya halaiki ya Wapalestina katika kambi za Sabra na Shatila ya kuingia katika Msikiti wa al Aqswa na kuuvunjia heshima msikiti huo mtukufu, iliwatia hasira Wapalestina na kuwafanya waanzishe maandamano na mapambano makubwa dhidi ya utawala huo wa Israel.
