Iraq yaonya dhidi ya kuibuka upya ISIS nchini Syria
(last modified Mon, 14 Apr 2025 13:06:51 GMT )
Apr 14, 2025 13:06 UTC
  • Iraq yaonya dhidi ya kuibuka upya ISIS nchini Syria

Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq, Fuad Hussein ameonya kuhusu kushadidi harakati za kundi la kigaidi na kitakfiri la Daesh (ISIS) katika nchi jirani ya Syria, kufuatia kuanguka kwa serikali ya Rais Bashar al-Assad mwishoni mwa mwaka jana.

Hussein ametoa onyo hilo wakati wa mkutano wa tano wa ngazi ya juu wa utaratibu wa usalama baina ya Iraq na Uturuki uliofanyika katika mji wa kusini magharibi mwa Uturuki wa Antalya jana Jumapili.

Mwanadiplomasia huyo mkuu wa Iraq ameonya juu ya "kuongezeka kwa harakati za Daesh nchini Syria, akitoa wito wa kuundwa kikosi cha oparesheni cha nchi tano kinachojumuisha Iraq, Uturuki, Jordan, Lebanon na Syria ili kukabiliana na tishio hilo."

Hali ya usalama nchini Syria bado ni tete baada ya makundi ya wanamgambo, wakiongozwa na Hay’at Tahrir al-Sham (HTS), kupindua serikali ya Assad mnamo Disemba 8, 2024.

Shirika la habari la Iraq la al-Maalomeh, likinukuu vyanzo vya habari vilivyozungumza kwa sharti la kutotajwa majina, liliripoti mapema mwaka huu kwamba, magaidi wa Daesh wanafanya harakati katika takriban mikoa kumi na mbili nchini Syria.

Duru hizo ziliendelea kusema kuwa, takriban nusu ya silaha zinazotumiwa na magaidi wa Daesh zinatengenezwa Marekani, na kuashiria kuwa wanamgambo hao wenye misimamo ya kufurutu ada wanashehenezwa silaha kwa siri.

Habari zaidi zinasema kuwa, magaidi wa Daesh wanatembea kwa uhuru katika maeneo mengi ya Syria, huku vikosi vamizi vya Marekani vikwatazama tu bila kuchukua hatua yoyote dhidi ya magaidi hao.