Maandamano makubwa yafanyika mjini Rabat, Morocco kuunga mkono Palestina
-
Maandamano makubwa yafanyika mjini Rabat, Morocco kuunga mkono Palestina
Mamia ya raia wa Morocco wameandamana na kukusanyika mbele ya jengo la Bunge mjini Rabat, wakitangaza himaya na uungaji mkono wao kwa watu wa Palestina na kulaani mzingiro wa utawala wa kizayuni wa Israel dhidi ya Ukanda wa Gaza.
Maandamano hayo yamefanyika kwa mwaliko wa "Kundi la Uchukuaji Hatua Kwa Ajili ya Palestina", ambapo washiriki wakiwa wamebeba mabango na maberamu walipaza sauti wakilaani kuendelea kulengwa kwa raia wa Palestina na kuonya dhidi ya kuendelea kuzuiwa misaada ya kibinadamu kuingia Gaza.
Waandaaji wa maandamano na mkusanyiko huo walitangaza kwamba, wamefanya hivyo kuitikia wito wa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS wa mikutano ya kila wiki katika nchi mbalimbali duniani kote kupinga kuendelea vita huko Gaza.
Aidha waandamanaji hao wametoa nara za kuunga mkono muqawama na mshikamano na Wapalestina, na kutoa wito wa kukomeshwa mashambulizi na mzingiro dhidi ya Ukanda wa Gaza.
Maandamano nchini Morocco yameshika kasi katika miaka michache iliyopita hususan tangu kuanza Vita vya Gaza na jinai kubwa zinazofanywa na utawala wa Kizayuni dhidi ya Wapalestina wasio na ulinzi.
Katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita, wananchi wa Morocco mbali na kulaani jinai za Israel dhidi ya Wapalestina, mara kadhaa wametoa mwito wa kufutwa makubaliano ya kuwa na uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Makubaliano ya kuweko uhusiano wa kawaida kati ya Morocco na utawala wa Kizayuni yalifikiwa mwezi Disemba 2020. Hata hivyo makubaliano hayo yameendelea kukabiliwa na upinzani mkali wa wananchi wa nchi hiyo.