Mkutano wa ECOWAS wafanyika Abuja, Guinea-Bissau na Benin katika ajenda
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i134292-mkutano_wa_ecowas_wafanyika_abuja_guinea_bissau_na_benin_katika_ajenda
Mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) umeanza rasmi Jumapili mjini Abuja, Nigeria, ukikusanya viongozi wa kikanda kujadili masuala nyeti yanayoathiri eneo la Afrika Magharibi.
(last modified 2025-12-14T09:38:58+00:00 )
Dec 14, 2025 09:38 UTC
  • Mkutano wa ECOWAS wafanyika Abuja, Guinea-Bissau na Benin katika ajenda

Mkutano wa kilele wa Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS) umeanza rasmi Jumapili mjini Abuja, Nigeria, ukikusanya viongozi wa kikanda kujadili masuala nyeti yanayoathiri eneo la Afrika Magharibi.

Kwa mujibu wa taarifa, mkutano huu unalenga zaidi matukio ya karibuni yanayohusisha Guinea-Bissau na Benin.

Katika ajenda ya mkutano huu, viongozi wanatarajiwa kushiriki katika mjadala maalum kuhusu mustakabali wa jumuiya, uwasilishaji wa Ripoti ya Mwaka 2025 kuhusu hali ya jumuiya, na mapitio ya mpango wa ECOWAS wa kurahisisha biashara ya kikanda ili kuongeza biashara ya ndani ya ukanda. Pia kutakuwa na taarifa kuhusu usalama wa kikanda, juhudi za upatanisho zinazoendelea, na mchakato wa kisiasa wa Guinea. Hatimaye, mkutano utahitimishwa kwa kupitishwa kwa tamko la mwisho na mkutano wa pamoja na waandishi wa habari.

Mwenyekiti wa kikao, Rais wa Sierra Leone Julius Maada Bio, yuko Abuja pamoja na marais wa Ghana, Senegal na Gambia. Hali hii inaashiria uzito wa mkutano huu ambao unatarajiwa kutoa mwelekeo mpya kwa mustakabali wa ECOWAS na mshikamano wa kikanda.

Wiki iliyopita ECOWAS ililaani vikali jaribio la mapinduzi nchini Benin na kueleza kuwa zinaiunga mkono serikali katika kudumisha utaratibu wa kikatiba.

Aidha mapemba mwezi huu, ujumbe wa upatanishi wa ngazi ya juu kutoka ECOWAS ulifanya mkutano na viongozi wa mpito wa Guinea-Bissau kujadili njia ya amani ya kumaliza mgogoro wa kisiasa uliosababishwa na mapinduzi ya kijeshi ya mwishoni mwa mwezi Novemba

Ujumbe huo ukiongozwa na Rais wa Sierra Leone na Mwenyekiti wa ECOWAS, Julius Maada Bio, ulikutana na viongozi wa mpito wakiongozwa na Rais wa Mpito Jenerali Horta Inta-A.

ECOWAS ilisitisha uanachama wa Guinea-Bissau katika vyombo vyake vya maamuzi kufuatia mapinduzi ya kijeshi yaliyomuondoa madarakani Rais Umaro Sissoco Embalo.