Feb 24, 2016 13:30 UTC
  • Wanajeshi watatu wauawa kaskazini mwa Mali

Watu wenye silaha wamefanya shambulio katika eneo la kaskazini mwa Mali na kuua wanajeshi watatu wa nchi hiyo.

Gazeti la Le Figaro la nchini Ufaransa limeripoti habari hyo na kumnukuu mwanajeshi mmoja wa Mali akisema leo kuwa, watu wenye silaha jana usiku walifanya shambulio katika kituo kimoja cha upekuzi kusini magharibi mwa eneo la Timbuktu karibu na mpaka wa Mali na Mauritania na kuua wanajeshi watatu na kuwajeruhi wengine wawili.

Wizara ya Ulinzi ya Mali imethibitisha habari hiyo ingawa hata hivyo haikusema sehemu hasa lilipotokea shambulizi hilo.

Serikali ya Mali ambayo hivi sasa iko katika mazingira magumu ya kutekeleza makubaliano ya amani na wapinzani, katika miezi ya hivi karibuni imekumbwa na mashambulio kadhaa ya makundi yenye misimamo mikali.

Eneo la kaskazini mwa Mali lilikuwa na machafuko tangu mwaka 2012 wakati makundi yanayotaka kujitenga yalipoteka maeneo kadhaa. Mwaka 2015, pande mbili za waasi na serikali zilifikia makubaliano ya amani baada ya kufanya mazungumzo ya muda mrefu na kumaliza mgogoro wa kaskazini mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.

Tags