Watu 35 wafariki dunia katika ajali ya basi nchini Zimbabwe
Kwa akali watu 35 wamefariki dunia baada ya basi walilokuwa wakisafiria kuhusika katika ajali mbaya ya barabarani nchini Zimbabwe.
Kanali ya televisheni ya serikali ya ZBC imetangaza habari hiyo leo Ijumaa na kueleza kuwa, ajali hiyo ilitokea usiku wa jana Alkhamisi katika mkoa wa Chipinge, kusini mashariki mwa Zimbabwe.
Paul Nyathi, Msemaji wa Naibu Kamishna wa Polisi nchini humo amesema, mbali na watu 35 kupoteza maisha kwenye ajali hiyo iliyotokea karibu na Soko la Jopa, wengine wasiopungua 71 wamejeruhiwa vibaya na wanatibiwa katika zahanati na hospitali zilizoko karibu na eneo la ajali. Amesema uchunguzi wa awali unaonyesha kuwa basi hilo lilikuwa limejaa kupidukia, kwani lilipaswa kubeba abiria baina ya 60 na 75.
Vyombo vya habari vya Zimbabwe vimeripoti kuwa, basi hilo lililohusika kwenye ajali hiyo lilikuwa limebeba waumini wa Kikristo wa Kanisa la Zion ambao walikuwa wanaelekea kwenye sherehe za Pasaka.

Madereva nchini Zimbabwe wametakiwa wachunge sheria za barabarani, wajali usalama wao, wa abiria na wa wapita njia ili kupunguza kiwango kikubwa cha vifo vinavyotokana na ajali za barabarani nchini humo.
Ajali mbaya za barabarani zinaripotiwa mara kwa mara nchini Zimbabwe, na aghalabu ya ajali hizo zinahusiana na kupakia abiria au mizigo kupita kiasi, barabara mbaya zenye mashimo, mwendo wa kasi na kupuuza sheria za barabarani.