Rais Pezeshkian akaribishwa rasmi nchini Belarus
Rais Alexander Lukashenko wa Belarus, siku ya Jumatano, alimkaribisha rasmi Rais Massoud Pezeshikian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran katika Ikulu ya Rais, ambaye amesafiri mjini Minsk akiongoza ujumbe wa ngazi za juu wa kisiasa na kiuchumi.
Katika hafla hiyo, kwanza wimbo wa taifa wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kisha wimbo wa taifa wa Jamhuri ya Belarus ulipigwa na kitengo cha sherehe kilichokuwepo katika uwanja huo. Baada ya hafla ya makaribisho rasmi, marais wa nchi mbili watakutana na kufanya mkutano wa pamoja wa wajumbe wa ngazi za juu wa Iran na Belarus. Katika safari hii, nchi mbili pia zitatia saini hati kadhaa za makubaliano na ushirikiano.
Mkutano na maspika wa mabunge ya seneti na la wawakilishi pamoja na kukutana na Wairani wanaoishi Belarus ni miongoni mwa mipango mingine ya safari hii ya Rais Pezeshkian. Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliwasili Belarus Jumanne usiku, kwa mwaliko rasmi wa Rais Alexander Lukashenko.