Save The Children: Njaa huko Gaza ni ya makusudi na ya kubuniwa
https://parstoday.ir/sw/news/daily_news-i130110-save_the_children_njaa_huko_gaza_ni_ya_makusudi_na_ya_kubuniwa
Katika taarifa yake siku ya Jumatano, mkuu wa shirika la kimataifa la Save the Children ameashiria hali mbaya ya Gaza na kusema njaa katika ukanda huo ni jambo lililopangwa, linalotabirika na linalosababishwa na mwanadamu.
(last modified 2025-08-28T08:14:31+00:00 )
Aug 28, 2025 08:12 UTC
  • Save The Children: Njaa huko Gaza ni ya makusudi na ya kubuniwa

Katika taarifa yake siku ya Jumatano, mkuu wa shirika la kimataifa la Save the Children ameashiria hali mbaya ya Gaza na kusema njaa katika ukanda huo ni jambo lililopangwa, linalotabirika na linalosababishwa na mwanadamu.

Katika taarifa yake Janti Soeripto, mkuu wa shirika la Save the Children ameitaja njaa kuwa sera ya makusudi na mbinu ya vita katika sura yake mbaya zaidi na kuongeza kuwa, utawala wa Kizayuni una uwezo wa kukomesha njaa hiyo, lakini umekataa maombi ya makumi ya mashirika yasiyo ya kiserikali ya kutaka kupeleka misaada huko Gaza.

Akisisitiza wajibu wa kimataifa wa kukomesha janga hilo, Soeripto amesema kuwa kila mtoa maamuzi duniani ana wajibu wa kisheria na kimaadili kuhusu suala hili. Mkuu wa shirika la kimataifa la Save the Children aidha ameeleza wasi wasi wake mkubwa kuhusu ongezeko la idadi ya watoto wanaotamani kufa huko Gaza na kusema kuwa watoto wengi wa Kipalestina wanawekwa katika vituo vya kijeshi vya Israel na kufikishwa mbele ya mahakama za kijeshi ambazo hazikidhi viwango vya kimataifa. Huku akizitaka nchi wanachama wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kusimamisha utumaji silaha kwa utawala ghasibu wa Israel na kujiepusha na misaada ya kijeshi kwa utawala huo wa kijinai, Janti Soeripto pia amesisitiza ulazima wa kuunga mkono mifumo ya uwajibikaji na kujiepusha kushiriki katika jinai za utawala huo.