Balozi wa Marekani Denmark alalamikiwa kuhusu juhudi za Marekani kujipenyeza kwa siri Greenland
Wizara ya Mambo ya Nje ya Denmark ilitangaza Jumatano kwamba imemwita balozi wa Marekani kufuatia ripoti za intelijensia zinazosema kwamba raia wa Marekani wamehusika kwa siri katika kuchochea upinzani dhidi ya mamlaka ya Copenhagen huko Greenland.
Gazeti la The New York Times liliandika siku ya Jumatano kwamba raia watatu wa Marekani wenye uhusiano wa karibu na utawala pamoja na rais wa zamani wa nchi hiyo wametuhumiwa kwa kuendesha "operesheni za kujipenyeza kwa siri" huko Greenland. Gazeti hili la Marekani limeongeza kuwa watu hao wamefanya safari kadhaa Greenland kwa ajili ya kukusanya taarifa na kuanzisha mawasiliano ya siri na mamlaka za mitaa ya eneo hilo.
Wakati huo huo, Shirika la Reuters pia limeandika kuwa madhumuni ya hatua hizi ni kuchochea upinzani dhidi ya utawala wa Denmark na kuhimiza kujitenga kwa Greenland na hatimaye kujiunga na Marekani. Pia limeripoti kuwa Wizara ya Mambo ya Nje ya Denmark imemwita balozi wa Marekani mjini Copenhagen na kuliita jaribio lolote la kushawishi mambo ya ndani ya Greenland kuwa jambo "lisilokubaliki kabisa".
Gazeti la New York Times limesisitiza kwamba Greenland ni eneo lililo na utawala wa ndani chini ya mamlaka ya Denmark na tajiri wa rasilimali za madini, ambayo yana umuhimu mkubwa wa kimkakati katika eneo la Aktiki. Mwishowe, gazeti hilo limesema kuwa mamlaka ya Denmark imeimarisha uhusiano wake na Greenland na kwamba inapanga kunufaika na msaada wa washirika wa Ulaya kwa ajili ya kukabiliana na juhudi hizo haribifu za Marekani.