Ansarullah yasambaza mkanda wa video unaoonesha namna inavyozamisha meli za maadui + Video
(last modified Thu, 20 Jun 2024 07:08:57 GMT )
Jun 20, 2024 07:08 UTC
  • Ansarullah yasambaza mkanda wa video unaoonesha namna inavyozamisha meli za maadui + Video

Afisa mmoja wa harakati ya Ansarullah wa Yemen amethibitisha kuwa harakati hiyo imesambaza mkanda wa video unaoonesha operesheni za harakati hiyo dhidi ya meli ya Tutor iliyokaidi marufuku ya kutoelekea kwenye bandari za utawala wa Kizayuni.

Afisa huyo wa Ansarullah ambaye hakutaka jina lake litajwe ameiambia televisheni ya Al Jazeera kwamba: Operesheni hiyo iliendeshwa dhidi ya meli hiyo ambayo ni ya kampuni ya Kigiriki na ambayo ilikaidi marufuku ya kutumia Bahari Nyekundu kuelekea kwa adui Mzayuni. Amesema: Meli hiyo ilipigwa katika operesheni ya hatua tano iliyotumia boti, droni na makombora.

Afisa huyo wa Ansarullah amesisitiza kwa mara nyingine tena kwamba: Mashambulizi dhidi ya meli za mashirika ambayo yana meli nyingine zinazokwenda kwenye bandari za adui yaani utawala wa Kizayuni wa Israel, kupitia Bahari ya Mediterania, yataendelea.

 

Amesisitiza pia kuwa operesheni hiyo iliyofanywa na harakati ya Ansarullah ni sehemu ya operesheni za kuunga mkono muqawama wa wananchi wa Ghaza na ni zawadi kwa Mujahidina katika siku ya Idul al-Adh'ha.

Kabla ya hapo, Shirika la Biashara ya Baharini la Uingereza lilikuwa limethibitisha habari hiyo kwa kusema: Inaonekana Wahouthi wa Yemen wamezamisha meli ya pili katika Bahari Nyekundu.

Kwenye kipindi cha miezi kadhaa iliyopita, na ikiwa ni katika kuwaunga mkono wananchi wa Ghaza, jeshi la Yemen limejiunga kwenye kuwaunga mkono kivitendo Wapalestina hasa wa Ghaza na harakati hiyo ya Kiislamu imekuwa ikizipiga meli za utawala wa Kizayuni wa Israel au meli yoyote inayoelekea kwenye bandari za utawala wa Kizayuni kupitia Bahari Nyekundu.